August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge wa Kibiti afunguka kuhusu mauaji

Askari wakiwa kaziki kuwasaka wauaji

Spread the love

ALLY Seif Ungando, Mbunge wa Jimbo la Kibiti, mkoani Pwani amesema mapambano ya kudhibiti mauaji yanayoendelea jimboni kwake yanaweza kurahishishwa kwa serikali kupeleka umeme katika vijiji mbalimbali ambavyo mpaka sasa havina umeme, anaandika Dany Tibason.

Mbunge huyo ambaye amekuwa kimya kwa muda, amevunja ukimya na kuishauri serikali ipeleke umeme katika Jimbo la Kibiti kwani giza lililopo wakati wa usiku linaweza kuwa chanzo cha ugumu wa mapambano ya vyombo vya dola dhidi ya watekelezaji wa mauaji hayo.

“Kutokana na mauaji yanayoendelea kutokea Kibiti, je, Serikali haioni umuhimu wa kupeleka umeme katika Jimbo hilo kwani inapofika usiku kunakuwa na giza totoro?” amehoji.

Akijibu swali hilo, Dk. Medad Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, amesema Serikali itapeleka umeme wa mradi wa REA katika vijiji vyote vikiwemo vijiji vilivyopo katika Jimbo la Kibiti.

“Utekelezaji wa mradi kabambe wa usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu umeanza kwa nchi nzima tangu Machi mwaka huu. Mradi huo unalenga kuongeza wigo wa usambazaji umeme katika vijiji ambavyo havijafikiwa na umeme ikiwa ni pamoja na vitongoji, taasisi za umma, mashine za maji na visiwani,” amesema.

Tangu kuanza kwa mfululizo wa mauaji wa watu katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji zaidi ya watu 40 wameuawa ambapo miongoni mwao 13 ni askari wa jeshi la polisi.

error: Content is protected !!