December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge wa Chadema aanika madudu ununuzi wa korosho

Spread the love

MBUNGE wa Jimbo la Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe amevunja ukimya juu ya manyanyaso wanayopata wananchi wa mikoa ya kusini katika mchakato wa Serikali kununua wa zao la korosho. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Katika taarifa ya Mbunge huyo kwa waandishi wa habari, imetaja matatizo nane yaliyotokea tangu kuanza kwa mchakato huo wa ununuzo mpaka sasa na athari tisa ambazo zinaweza kutokea.

Hii hapa chini taarifa kamili ya Mbunge huyo;

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

4 Januari 2019

Ndugu wanahabari nawatumia taarifa hii, kwa nia ya kufikisha kilio cha wakulima wa korosho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Dk,John Pombe Magufuli kwasababu ndio zao tegemeo la kiuchumi kwa sasa.

Kama mnavyojua mkoa wa Mtwara umekuwa ukiongoza kwa kuzalisha korosho nyingi ikifuatiwa na mkoa wa Lindi,Ruvuma na Pwani pamoja na mikoa mingine mipya ambayo inaongezeka siku hadi siku.

Mtakumbuka baada ya mvutano kati ya serikali na wafanya biashara (wanunuzi wa korosho) baadae serikali iliamua kutangaza kuzinunua korosho zote kwa Tsh.3,300/-kwa kilo.

Zoezi hili lilifanyika kwa maamuzi ya haraka kabla ya kupata ushauri wa kitaalamu lakini pia utafiti wa kina wa namna ya kufanikisha zoezi hili la ununuzi wa korosho ikiwa ni pamoja na kupata uhakika wa soko la korosho na taratibu zingine.

hata hivyo, itakumbukwa wakati huo wanunuzi na makundi yao walishauri namna bora ya kutekeleza maelekezo hayo bila mafanikio.

Serikali ilifanya uamuzi wa kununua korosho kwa kutumia tafiti ambazo hazikuwa sawa, wakati huo nguvu ya soko haikuzingatiwa (soko ka dunia) na badala yake suala hili lilijawa na mihemko, pamoja na nia njema ya serikali ya kuwasaidia wakulima, lakini sasa imekuwa ni kilio kila kona badala ya furaha.

Mfano halisi ni pale Mheshimiwa Rais alipodanganywa na yeye akatangaza hadharani kuwa korosho zote zinazozalishwa nchini zitabanguliwa hapa nchini kwa kutumia viwanda vilivyopo ikiwemo kiwanda cha Buco Lindi ambacho baadae kiligundulika hakina uwezo wa kubangua korosho na hata vipuli vyake vilishanyofolewa, na kiwanda kiwanda icho sasa kinatumika ghala la kuifadhia mazao, hii ni sawa na kiwanda kilichoko Masasi, nacho kinatumika kama ghala na bado shauri lake liko mahakamani.

Haya yote yalikuwa ni matumaini hewa kwa wakulima wetu, na sasa hali halisi imeanza kujionyesha.

Wakati wa kikao cha mashauriano cha Mkoa wa Mtwara (RCC) tulipokea taarifa kwamba kwa mwaka nchi ina uwezo wa kubangua tani 20,000 tu kati tani 270,000 zinazotarajiwa kukusanywa.

Taarifa hii inapingana na taarifa ya Waziri wa viwanda kwamba tani 100,000 zitabanguliwa na hivyo serikali sasa inatafuta wadau ili wawezi kununua ziada ya tani 150,000.

Hivyo ndugu wanahabari, nawaanfikia leo ili kutoa mrejesho wa yanayoendelea katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani kwa wakulima baada ya kufanya uchunguzi wangu binafsi kama Mwakilishi wa Wananchi wa Jimbo la Ndanda ambao na wao wako katika Kilio cha kutolipwa.

Ifahamike kwamba, baadhi ya wakulima wanalipwa, wale wanaizalisha zaidi ya tani 1.5 wao hawalipwi, wakiwemo makundi ya Wazee, wajane na warithi. Ivi kuwaongezea uchungu wa maisha kwa kisingizio cha uhakiki,

Yafuatayo ni matatizo yaliyopo kwenye tasnia ya Korosho kwa sasa

1. Utaratibu wa malipo umekuwa wa kusuasua sana tofauti na taarifa alizopewa Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu.

2. Wakati kinachodaiwa kuwa zoezi la uhakiki kikiendelea kuna viashiria vya rushwa kutoka kwa wahakiki.

3. Wakulima wamegawanywa kwa makundi makundi na hivyo kuwafanya wawe wanyonge zaidi

4. Taarifa za malipo zikekuwa za siri kiasi kwamba hata viongozi wa vyama vya msingi hawana taarifa wala kufahamu kinachoendelea juu ya wakulima waliokusanya korosho maghalani, ivyo kuhatarisha uhai wa vyama ambavyo vitakumbwa na madeni makubwa, yakiwemo ya wabebaji na wasafirishaji.

5. Matumizi makubwa ya nguvu kutoka vyombo vya ulinzi na usalama, jambo hili liko maeneo mengi, kubwa zaidi ni tukio lililotokea Nachingwea, viongozi wa vyama vya msingi wamepigwa na wanajeshi kwa kushirikiana na polisi ofisini kwa Katibu tawala (DAS), ushahidi upo na waliofanya tukio hilo wanafahamika kwa majina

6. Uwezo mdogo wa wahakiki na ujuzi kuhusiana na zao la korosho, wahakiki nao wako mafunzoni, badala ya kutekeleza wajibu

7. Malalamiko yanayotolewa chinichini kutoka kwa wasimamizi wa zoezi la uhakiki, kuhusu posho zao na stahiki nyingine, ivyo kuongeza gharama za uendeshaji, overhead cost

8. Kuna dalili zote za kutokea kwa utaifishaji wa mali za wananchi kwa kisingizio cha kukomesha biashara ya kangomba. Tumesikia mara kadhaa Mheshimiwa Rais akisema kuwa korosho zote zenye dalili za kupatikana kwa njia ya kangomba hazitalipwa, na leo kayarudia maneno hayo tena Ikulu

Swali la kujiuliza kama wauzaji wa korosho hizo hawatalipwa na korosho zao zimechukuliwa na serikali, je hii tunaita nini?
Ni kweli kwamba hakuna wachuuzi wa mazao mengine zaidi ya korosho.

Tusitumie matatizo kwa kukata matawi ya tatizo bali tutatue matatizo kwa kung’oa mizizi ya tatizo.

Ni vyema serikali kufatuta mzizi wa uwepo wa biashara ya kangomba ambao ulisababishwa na udhaifu wa mifumo ya serikali katika kusimamia mazao ya wakulima hasa zao la korosho.

Hivyo ndugu waandishi, kutokana na masuala ya msingi niliyoyataja yanaweza kuwa na athari kubwa sana kwa mwananchi mmoja mmoja lakini athari kubwa iko kwa Taifa.

Naomba niwatajie athari chache zinazoweza kujitokeza sasa hivi na baadae….

1. Halmashauri zetu zitashindwa kujiendesha kwa sababu zinategemea kwa kiasi kikubwa mapato yatokanayo na mazao ikiwemo korosho, mtakumbuka kwamba mbaazi haikuwa na soko zuri msimu uliopita.

2. Kuharibika kwa korosho zilizoko maghalani kwa kunyeshewa na mvua, hasa zile zilizoko mikononi mwa wakulima, na hivyo kupoteza ubora wake ambao ndio sifa kuu ya korosho ya nchi yetu.

3. Wakulima kudhalilishwa kwa kushindwa kujimudu maisha yao ya kawaida mfano kulipia ada za watoto (private schools) na michango mbalimbali hii pia itasababisha kushuka kwa elimu, lakini pia wakulima hawa hawa wanashindwa kuandaa mashamba yao kwa ajili ya msimu ujao, ivyo kupunguza uzalishaji, na baadae kipato kuendelea kushuka

4. Kupoteza mapato kwa serikali kwa maana ya Export Levy na Export Revenue hivyo kushusha thamani ya shillingi, na pia kupoteza imani kwa wafanya biashara wa nnje na wa ndani wa mazao.

5. Kupungua kwa mzunguko wa pesa kwenye mabenki, na hata mitaani kwa vendors, kwa mfano miamala ya fedha kwenye simu.

6. Bidhaa kudorora madukani, hasa maduka ya vifaa vya ujenzi na vyakula kwasababu wafanyabiashara wakishajua ni wakati gani wakulima wanahitaji biadhaa fulani fulani.

7. Kujengeka kwa chuki kati ya wananchi na serikali hasa kwa wale ambao watadhulumiwa korosho zao.

8. Kudorora kwa shughuli za maendeleo katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ambao kipindi kama hiki wananchi wanakuwa na kazi nyingi za maendeleo yao hasa ujenzi na uboreshaji wa makazi, na miundombinu mingine yakiwemo madarasa zahanati nk

9. Mwisho vitendo vya kiuhalifu vinaweza kuibuka au kuongezeka sababu tunajua korosho inayolimwa Mtwara inatoa ajira mpaka kwa watu ambao mikoa yao hailimi korosho mfano wabebaji korosho wanakuja kila msimu na ndio ajira yao na sasa haipo wanaweza kufanya lolote.

Mnafahamu kwamba kwa sasa ivi baada ya shughuli za utafutaji na uchimbaji wa gesi kutokuwa kipaumbele cha serikali hii, tulifikiri kwamba korosho ingeweza kutuinua sisi wanyonge wa Kusini, tofauti na matarajio yetu, hata kile kidogo tulichonacho, nacho kuna dalili ya kukichukua.

Hivyo ndugu wanahabari, pamoja na mengine mengi.

Tumemsikia Mheshimiwa Rais kila mara anajiita kuwa ni Rais wa Wanyonge
Je hiki kinachoendelea ni kutetea wanyonge au kuzidi kuwadidimiza wanyonge katika Lindi kubwa la umaskini?

Nasikitika sana kuwa baadhi ya viongozi aidha kwa makusudi au kuamua kumdanganya Mheshimiwa Rais wanapeleka taarifa za ununuzi wa korosho na malipo yake kuwa yanaendelea vizuri jambo ambalo sio kweli.

Ni wakati sasa wa Mh Rais kutembelea mikoa ya Kusini na kuwapa wananchi nafasi ya kuzungumza ili ajionee mwenyewe ni kitu gani kinaendelea kwa lengo la kumsaidia mkulima na si vinginevyo, tunafahamu katika hatua hii watu wengi wanaweza kutayarishwa kukudanganya na kukusifia,
kuwa makini Baba

Imeandaliwa na;

Cecil David Mwambe (Mb)

Mbunge Jimbo la Ndanda

error: Content is protected !!