July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge wa Chadema aahidi hospitali Arumeru

Spread the love

MGOMBEA Ubunge jimbo la Arumeru Magharibi kwa tiketi ya Chadema, Gibson Meiseyeki amesema kuwa atahakikisha analibadili jimbo hilo kwa kuweka miundombinu ya barabara, hospitali kubwa ya kisasa na maji katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto hiyo kwa muda mrefu. Anandika Ferdinand Shayo, Arusha … (endelea).

Aidha amesema kuwa, jimbo hilo ambalo kwa muda mrefu lilikuwa likiongozwa na CCM limekuwa likikabiliwa na changamoto nyingi ambazo zimewapelekea wananchi wake kuishi mazingira magumu hadi sasa, ila kwa sasa hivi Chadema wamejipanga kushika dola kuanzia urais hadi udiwani.

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi kwenye kampeni katika kata ya Kisongo, Arumeru, ambapo aliwaahidi kuwajengea hospitali kubwa ya kisasa ili itoe huduma katika jimbo hilo.

“Jamani mimi mnanijua vizuri nimefanya mambo makubwa nikiwa diwani wa kata ya Oltoroto ikiwemo kujenga shule ya kisasa ya ghorofa moja katika kata yangu kwa kutumia wafadhili ambao niliwatafuta kwa nguvu zangu mwenyewe sasa nitafanya makubwa zaidi ya haya endapo nitachaguliwa kuwa mbunge wenu,” amesema Meiseyeki.

Aliongeza kuwa, kata hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya maji safi na salama hali ambayo inawafanya wakina mama wa kimasai kutembea na punda umbali mrefu kwa ajili ya kusaka maji safi na salama, ambapo aliahidi kuwavutia maji ili waondokane na changamoto hiyo kwani wakichagua viongozi wa Chadema watakuwa wamechagua mabadiliko ya maisha yao.

Aliwataka wananchi hao kuwa makini na vyama vya siasa vinavyowagawia sukari, na vipande vya kanga ili wawachague, kwani kukichagua chama cha namna hiyo, kwani hao ni wadanganyifu na ndiyo maana wanaendelea kubakia maskini na hakuna maendeleo yoyote.

Kwa upande wa mgombea udiwani kata ya Kisongo, Joseph Laizer maarufu kama ‘Bekar’ amewaahidi wananchi hao kuwafanyia maajabu katika kata hiyo endapo atachaguliwa kuwa diwani wa kata hiyo na kuahidi kuanza kuwashughulikia watendaji wote wanaokula fedha za maendeleo ya kata.

Bekar amesema, yeye ni mzoefu wa muda mrefu na anafahamu jinsi ambavyo fedha za maendeleo zinavyoliwa na watendaji, hivyo jambo la kwanza atakaloanza nalo ni kuhakikisha fedha zote zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi zinatumika ipasavyo.

Mwenyekiti wa Balaza la Wanawake Chadema (BAWACHA) jimbo la Arumeru Magharibi, Nuru Ndossi amewataka wananchi hao hasa wanawake kutokubali kurubuniwa na sukari nusu kilo ili kuichagua CCM na badala yake hivyo amewataka kubadilika sasa na kutoa kura zote Chadema.

error: Content is protected !!