January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge wa CCM aishambulia Serikali

Spread the love

MBUNGE wa Mtera, Livingston Lusinde (CCM) ameishambulia Serikali yake kwa kitendo cha kuwanyanyasa waendesha pikipiki maarufu kama ‘boda boda’. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Lusinde amesema  Serikali  inatakiwa kuingilia kati zoezi la kamata kamata ya waendesha boda boda ili waweze kufanya kazi katika mazingira rafiki kama walivyoahidiwa wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2015.

Mbunge huyo amesema ni aibu kwa Serikali na viongozi wake na wanasiasa ambao wakati wa kampeni walikuwa wakiwaona waendesha bodaboda kama watu muhimu lakini baada ya uchaguzi wametelekezwa kwa kutosa mtetezi.

Amesema wakati wa kampeni boda boda waliahidiwa kuboreshewa mazingira ya kufanyia kazi ikiwa ni pamoja na kutokamatwa bila ya sababu ili waweze kujiiuna kiuchumi.

Lusinde ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa kuhusu kero ha waendesha boda boda kukamatwa.

Amesema ni vyema serikali ikiangilia kati hali hiyo kwa sababu inawafanya waendesha boda boda kukosa imani na ahadi walizoahidiwa wakati wa kampeni.

“Ukiona mtu anaonewa na wewe unakaa kimya utakuwa unaungana na mtu anayemuonea, mimi nimeamua kusema niiombe Serikali katika hili, maana vijana wamejiajiri katika sekta hiyo lakini mazingira wanayofanyia kazi ya kukamatwa kamatwa yatawafanya kurudi kwenye vijiwe vya uhalifu,” amesema Lusinde.

Alibainisha wakati wa kampeni Rais Dk. John Magufuli aliahidi kutoa uhuru mkubwa sana kwa watu wa hali ya chini wakiwemo boda boda kwamba waliahidiwa kusaidiwa na kuwezeshwa ili wawe sawa na watu wengine.

Amesema katika Mkoa wa Dodoma na nchi nzima kinyume na kauli ya Rais kumekuwepo na kamata kamata kubwa sana na kutozwa faini ambazo zingine zimeongezeka ikiwemo ya kuweka namba za pikipiki kwenye kofia zao.

“Sasa haya makofia yaandikwe namba yasipoandikwa unakutana na faini, hawa boda boda wamekuwa wakilipa faini hadi makosa manne kwa siku, wengine mpaka wanafikia kutoa Sh. 250,000, sasa jamani kwa hali hii ndivyo tulivyowaahidi kuwarahisishia maisha?” amehoji Lusinde.

Alimuomba Waziri wa mambo ya ndani na Waziri wa Fedha kuingilia kati kusaidia kwa sababu vijana wengi hata hizo boda boda sio zao, wanafanya kazi katika mazingira magumu huku familia zikiwasubiri.

Akizungumzia kamata kamata hiyo, Mkuu wa kitengo cha Usalama barabarani mkoa wa Dodoma, Nuru Seleiman, amesema zoezi hilo ni la wiki mbili ambapo mpaka sasa pikipiki 777 zimekamatwa kufuatia makosa mbalimbali.

Amesema lengo la msako huo ni kurudisha heshima ya waendesha pikipiki barabarani kutokana na kutozingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.

Mkuu huyo amesema asilimia 60 ya ajali zilizotokea mwaka jana zilisababishwa na pikipiki kutokana na waendeshaji kutofuata sheria.

“Asilimia 50 ya vifo vilivyotokana na ajali za pikipiki vilitokana na waendeshaji na abiria kutovaa kofia ngumu, zoezi ni endelevu na tumelenga kupunguza vifo, ajali na matukio ya kiuhalifu,” amesema Seleiman.

Amewataka waendesha pikipiki kuhakikisha wanakuwa na leseni za biashara, leseni za udereva na kuvaa makoti maalum ya kuendeshea na kofia ngumu kwa mujibu wa kanuni zote za usafirishaji.

Aidha amesema katika operasheni hiyo jumla ya pikipiki 578 zimelipa faini kwa makosa mbalimbali huku zingine zikilipa faini ya zaidi ya kosa moja.

error: Content is protected !!