December 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge: Serikali acheni kuikwapua mifuko

Mwenyekiti wa CUF, wilaya ya Lindi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini, Salum Barwany.

Spread the love

MBUNGE wa Lindi Mjini, Salum Baruwany ametaka serikali iache utamaduni mbaya wa uingiliaji mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuipa fursa ya kisheria ya kuimarisha huduma kwa wafanyakazi wanaotoa michango yao kwenye mifuko hiyo. Anaandika Jabir Idrissa.

Baruwany ambaye ni mbunge kupitia Chama cha Wananchi (CUF), amesema bungeni leo jioni katika kujadili taarifa ya kamati maendeleo ya jamii, kwamba uingiliaji wa mifuko hiyo unaofanywa na serikali unaidhoofisha na kuhatarisha uendelevu wake.

Amesema wakati mafao ya wafanyakazi wastaafu hayaongezeki kwa kiwango kinachoridhisha, serikali inaingilia mifuko na kukwapua fedha za wafanyakazi, jambo lisilokubalika.

“Uingiliaji huu ukomeshwe ili kuiepusha mifuko na kifo cha kudumu. Serikali ambayo imetakiwa kutoa asilimia 40 ya mtaji wa kutekeleza mradi wa nyumba za kibiashara kijiji cha Kigamboni pamoja na NSSF, mpaka sasa haijatoa fedha yoyote. Naona itafika mwisho mradi utakuwa ni wa NSSF peke yao,” amesema.

Baruwany ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino), akisikitishwa na kitendo cha serikali kudaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii nchini zaidi ya Sh. 1.2 Trilioni, amesema kuanzia sasa, ni bora uwepo utaratibu wa serikali kueleza hasa fedha zichukuliwe kwa kazi gani na ni nani ameidhinisha badala ya kuendekeza mtindo wa kukwapua fedha za wafanyakazi.

Rai ya mbunge huyo inazingatia ukweli kwamba serikali imeshindwa kulipa fedha nyingi ilizozichukua kwenye mifuko hiyo kwa ajili ya kufanya matumizi yake, achilia mbali mabilioni ya shilingi yaliyotumiwa na mifuko kutekeleza miradi ya maendeleo kama ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Taifa Dodoma (UDOM), daraja la Kurasini/Kigamboni pamoja na nyumba za bei nafuu.

Kushindwa kwa serikali kurejesha fedha za mifuko kwa wakati, kumekuwa kukilalamikiwa na asasi za kiraia, wafanyakazi wenyewe na vyama vyao makazini. Eneo hili limekuwa likipigiwa kelele mara kwa mara na wabunge kama linavyofuatiliwa kwa karibu na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali – Controller and Auditor General (CAG) na kubainisha upungufu huo kwenye taarifa zake za kila mwaka.

Katika taarifa yake ya mwisho, CAG amesema hali ya mifuko inasikitisha kwani baadhi yao uendelevu wake upo hatarini kutokana na fedha nyingi kuwa mikononi mwa serikali.

Mifuko ya hifadhi ya jamii nchini ni NSSF, PSPF, PPF, GEPF pamoja na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).

error: Content is protected !!