August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge Segerea anachanganya wananchi

Spread the love

NIMEKUWA mkazi wa Segerea kwa muda mrefu, lakini kwa sasa naona hofu kwa wakereketwa wa maendeleo inavyowatawala, anaandika Mwandishi Wetu.

Hofu hiyo inahusu matumizi ya Fedha za Mfuko wa Jimbo lao kama zitatumika kwa namna ilivyokusudiwa na sheria inavyoelekeza. Hofu hii haijapata majibu.

Kwa namna ilivyo, fedha hizo kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya jimbo zinazosimamiwa na sheria Na. 16 ya mwaka 2009 (The Constituencies Development Catalyst Fund Act, Na.16 of 2009), inamtaka mbunge kuelekeza fedha hizo kwenye miradi inayoibuliwa na wananchi wenyewe katika jimbo husika.

Kwa mujibu wa sheria na mwongozo wa mfuko wa jimbo, imetaka kuundwa kwa kamati ya usimamizi wa fedha za mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo.

Kamati hiyo itakuwa na wajumbe sita pamoja na mbunge mwenyewe. Kamati hiyo inaundwa na Mbunge wa Jimbo ndiye Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Mchumi wa Manispaa ya Ilala ambaye ndiye Katibu wa Kamati, wajumbe ni madiwani wawili wa kata (Me/Ke), watendaji kata wawili (Me/Ke) na mwakilishi wa taasisi zisizo za kiserikali (NGos).

Historia inatueleza kuwa, mfuko huo katika Jimbo la Segerea lililopo kwenye Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam umekuwa ukikumbwa na mkanganyiko baina ya mbunge na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa.

Mkanganyiko huo umekuwa ukisababisha ufanisi wa matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo kutia shaka katika manispaa si Ilala pekee hata kwenye manispaa zingine nchini.

Ni kwa kuwa, wabunge wengi wamekuwa wakizitumia fedha hizo katika maswala ya kisiasa zaidi kuliko mahitaji halisi ya  miradi ya maendeleo ya wananchi. Hali hii pia imeonekana kwa wananchi wa Jimbo la Segerea

Hofu ya wananchi wa Jimbo la Segerea imekuja Mara baada ya Bonna Kaluwa, Mbunge wa Segerea kuanza ziara ya kutembelea miradi inayosimamiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala chini ya Mstahiki Meya, Charles Kuyeko.

Kuyeko pia ni Diwani wa Kata ya Bonyokwa akisaidiwa na Omary Kumbilamoto, Naibu Meya pia Diwani wa Vingunguti na kuwa, Kaluwa amekuwa akijinasibu kwamba ndio muhusika wa miradi hiyo.

Sheria ya mfuko wa kuchochea Maendeleo ya Jimbo (CDCF) kifungu cha 12 inaeleza wazi kuwa, orodha ya miradi inayotekelezwa na fedha za mfuko wa jimbo ni ile inayoibuliwa na wananchi wanaoishi katika jimbo husika.

Sheria hiyo hiyo kifungu cha 10 (4) kinaitaka kila kata kuandaa miradi inayopewa kipaumbele na kuiwasilisha kwenye kamati ya mfuko wa jimbo kwa ajili ya kuidhinishwa au kutoidhinisha miradi hiyo.

Mpaka sasa hakuna diwani yeyote wala kamati ya maendeleo ya kata yoyote ile katika Jimbo la Segerea iliyowasilisha orodha ya miradi hiyo mbele ya kamati ya fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo inayoongozwa na mbunge Bonna.

Hii inatokana na kwamba mbunge na kamati yake hawataki kuweka mambo wazi na hali hii imeanza kuwatia hofu wananchi wa Segerea kama fedha hizo zitatumika kwenye miradi ya maendeleo ama la.

Moja ya miradi ambayo Bonna amekuwa akisema anaisimamia ni ujenzi wa Daraja la Bonyokwa -Kinyerezi.

Lakini ukweli unaoelezwa ni kuwa, daraja hilo liko chini ya Tanroad, kutokana na ujenzi wake kusuasua Kuyeko, Meya wa Ilala alimwandikia barua Meneja wa Tanroads kuomba kuazima daraja la chuma ili kuwanusuru wananchi wa Kata ya Bonyokwa.

Tanroad walikubali kumwazima daraja hilo pamoja na injinia wa kuunganisha vuma vya daraja hilo.

Katika kuonyesha kuwa hofu ya wanasegerea ina mashiko, ni hivi karibu wakati Bunge la Bajeti likiendelea, Bonna alisikika akizungumza bungeni, mjini Dodoma kuwa, amekarabati Machinjio ya Vingunguti.

Hatua hiyo imetushitua wakazi wa Segerea hususani wananchi wa Kata ya Vingunguti ambao walishirikiana na diwani wao Kumbilamoto kuhakikisha manispaa inatoa fedha kwa haraka kwa ajili ya kukarabati machinjio hayo.

Ni wazi kabisa kwa nafasi yake ya ubunge Bonna anaingia kwenye Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Ilala, hivyo anajua wazi kuwa machinjio hayo yametengewa jumla ya Sh.650,000,000 fedha za ndani za manispaa.

Sehemu ya fedha hizo ndiyo iliyotumika kukarabati machinjio hayo baada ya kufungiwa kutokana na miundombinu mibovu na uchafu uliokithiri.

Katika ukarabati huo, hakuna sehemu ambayo fedha ya jimbo ilitumika. Kwa kuwa, wananchi wapo njia panda kutokana na kauli za Bonna, ni wakati sasa mbunge huyo akajitokeza na kueleza mwelekeo ya fedha za jimbo ni upi.

 

error: Content is protected !!