January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge Rweikiza “kitanzini” Bukoba

MBUNGE wa Bukoba Vijijini, Jason Rweikiza

Spread the love

MBUNGE wa Bukoba Vijijini, Jason Rweikiza (CCM) anatuhumiwa kutumikisha wafanyakazi katika shule yake ya Rweikiza English Medium and Nursery School kwa kutokuwapo mikataba ya ajira. Anaandika Edson Kamukara … (endelea).

Kutokana na hilo, wafanyakazi ambao ni pamoja na walimu wapatao 30, hawalipi kodi (PAYE), hawachangii mafao ya pensheni katika mfuko wowote wa jamii; na wanawake hawapati likizo ya uzazi.

Shule hii ipo eneo la Kyetema-Mchangani, yapata kilometa 15 nje ya mji wa Bukoba, kwenye barabara iendayo Biharamulo.

Rweikiza ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ambaye wafanyakazi wake wanadai “angekuwa anaelewa na kuthamini haki.”

Wafanyakazi hao, wasio na mikataba ya ajira, wasiolipa kodi ya PAYE na wasiopata likizo ya uzazi; ndio wameiwezesha shule ya Rweikiza, iliyoanzishwa mwaka 2010, kuwa na ufaulu wa juu katika matokeo ya mtihani wa Darasa la Saba.

Katika matokeo ya 2014, shule hii imekuwa ya kwanza kati ya shule 145 za wilaya ya Bukoba Vijijini; ikaibuka ya pili kati ya shule 909 za mkoa wa Kagera na ya 13 kitaifa kati ya shule 15,867.

“Tunaogopa kudai haki zetu kwa nguvu. Tutafukuzwa kazi. Lakini kubwa zaidi ni kutopata hata nafasi ya kuzungumza na Rweikiza kuhoji unyanyasaji huu,” ameeleza mwalimu.

Mkuu wa shule hiyo, Baraka Mwambinga anakiri Rweikiza kutokutana na wafanyakazi. Anasema “…hajataka kukutana nao, ila simu yake iko wazi na namba yake wanaijua; anayemhitaji anaweza kumpigia simu wakati wowote.”

Lakini Rweikiza hakubaliani na madai hayo. Katika mahojiano na gazeti hili amesema, “NSSF na Bima ya Afya wanazo. Wanapata likizo za uzazi na wanalipwa. Mishahara ni ya kawaida – mikubwa na midogo – kutegemea kazi ya mtu, elimu, madaraka, uzoefu, uwezo wa kulipa na mengineyo.”

MwanaHALISIOnline limedokezwa kuwa wafanyakazi wa shule ya Bukoba ndio pekee wenye malalamiko. Wenzao katika shule tatu za Rweikiza za jijini Dar es Salaam “hawasikiki kudai chochote.”

Rweikiza anamiliki pia shule za msingi na sekondari za St. Anne Maria, Sunshine na Brilliant zilizopo Dar es Salaam.

“Hatuna mikataba ya ajira. Makubaliano yanafanyika kwa mdomo. Mshahara wa chini hapa kwa mwezi ni Sh. 200,000 na kima cha juu ni Sh. 350,000 kwa walimu,” ameeleza mwalimu mwingine.

Amesema watumishi wengine – wapishi, mweka fedha, mhasibu, madereva, walinzi, wafanya usafi na matroni – nao wanalalamika kama walimu; lakini viwango vyao ni vya chini kuliko vya walimu.

“Fikiria mtu anayepata mshahara wa Sh. 100,000. Atoe nauli ya Sh. 2,000 kwa siku (sawa na sh. 60,000) kwa mwezi… anabaki na nini? Rweikiza haruhusu mfanyakazi kupanda gari la shule. Akibainika anafukuzwa kazi,” analalamika mfanyakazi.

Wafanyakazi wanaelewa kuwa sheria ya ajira inataka mfanyakazi mjamzito apewe likizo ya uzazi ya miezi mitatu na malipo; “…lakini hapa mzazi anapewa mwezi mmoja na ukiisha haruhusiwi kuja na mtoto kazini, isipokuwa atakwenda kunyonyesha saa nane mchana.”

Lakini lini wafanyakazi wamekutana na Rweikiza na mara ngapi kumweleza matatizo yao? “Utaanzia wapi? Anakuja hapa. Anazunguka eneo lake lote; kisha anazungumza na ‘watu wake’ na kuondoka,” anaeleza mwalimu.

Taarifa za shuleni hapo zinaeleza kuwa suala la kutolipa michango NSSF lilifichuka baada ya watendaji wa shirika hilo kutembelea shule 28 Februari mwaka huu, na kuwaelimisha wafanyakazi kutambua wajibu wa mwajiri kupeleka michango hiyo.

“Tulipigwa butwaa. Tukauliza haki hizi tutazipataje ikiwa hatuna mikataba ya maandishi wala vitambulisho vya kazi. Tuliwaeleza NSSF kwamba hata mishahara imeanza kupitia benki Mei 2014; awali tulipokelea dirishani,” ameeleza mfanyakazi.

Kwenda kwa NSSF shuleni Bukoba sasa kumeamsha watumishi. Kuna taarifa kuwa wanapanga kuiomba serikali kuingilia kati ili wapate kile walichokwishapoteza na kuwekwa utaratibu utakaowahakikishia haki.

Angalia hata hili, mfanyakazi anaonesha kitanda katika bweni, “Idadi ya wanafunzi imeongezeka. Watoto wanalazwa kitandani wawili-wawili. Ni rahisi hata kuambukizana magonjwa.”

Mwalimu mkuu wa shule, Baraka Mwambinga ameiambia MwanaHALISIOnline, “…kuhusu NSSF, ni kweli hazikuwa zikipelekwa; lakini hivi karibuni tumeanza kufanya utaratibu.”

Alipoulizwa iwapo haoni ni kinyume cha taratibu za ajira, alisema “…unajua, awali shule ilianza kama huduma kwa majirani wasio na uwezo wa kupeleka watoto katika shule za nje za gharama kubwa. Sasa tumepanuka tunaboresha.”

Kuhusu wanafunzi kulazwa wawili-wawili kitanda kimoja, Mwambinga alisita kidogo, kisha akasema madai ya wanafunzi “kulazwa wawili-wawili siyo ya kweli. Tuna vitanda vya kutosha…hilo tatizo halipo.”

Kuhusu walimu, Mwambinga amesema waliomweleza mwandishi kinachoitwa malipo duni kwa walimu, walimwambia uongo. “…hapa walimu wanalipwa vizuri na kupata haki zao zote.”

MwanaHALISIOnline lilipomtafuta Rweikiza kwa simu hakupatikana; simu ilikuwa ikiita bila kupokelewa. Lakini alipopelekewa ujumbe wa simu, alifunguka.

Akijibu malalamiko ya wafanyakazi, Rweikiza aliandika sms, “…licha ya kuwa mimi ni mwanasheria mwandamizi, ni mtu mwenye umri mkubwa, ni kiongozi mkuu wa kisiasa na kijamii. Hakuna wanafunzi wanaolala wawili kitandani.”

Aliandika, “Hakuna dhuluma nyingine au yoyote ile; hayo unayosema yangekuwa ya kweli au hata nusu yake, shule isingekuwa bora kama ilivyo hadi inakuwa ya kwanza wilayani na mkoani ya 11 kati ya shule 16,000 Tanzania nzima.”

“Wafanyakazi wasingekuwa na ari ya kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa. Baadhi ya wafanyakazi wanapewa nyumba za shule bure bila malipo. Wanapewa chakula cha mchana bure bila malipo,” alieleza.

Katika majibu hayo kwa njia ya sms, Rweikiza anasema kama wafanyakazi wangekuwa wanafanyiwa “dhuluma” wasingekubali kuajiriwa au kuendelea kuajiriwa kwa sababu ni hiari yao na hawashurutishwi.

“Pia wafanyakazi wanaopata matokeo mazuri katika kazi zao wanalipwa bonasi kubwa-kubwa kulingana na matokeo ya kazi zao,” amesema.

Uchunguzi wa MwanaHALISIOnline umebaini kuwa wafanyakazi wanaopewa nyumba za shule bure ni walimu wanane tu; tena wanaotoka Uganda. Hawa wanapewa pia chakula cha mchana bure.

Ada ya mwanafunzi wa kutwa na wa bweni, wa madarasa ya awali katika shule yake, ikiwa ni pamoja na usafiri, haizidi Sh. 1,300,000.

Ada kwa darasa la kwanza hadi la saba zinatofautiana, lakini hazizidi Sh. 1,500,000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi.

error: Content is protected !!