July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge, RC wavurugana

Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana

Spread the love

STANSLAUS Mabula, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza na John Mongella, mkuu wa mkoa huo wanavurugana, anaandika Moses Mseti.

Viongozi hao wanaoitumikia Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameingia katika mzozo kuhusu kuwaondoa wafanyabiashara ndogo ndogo (machinga) ifikapo Agosti mosi mwaka huu.

Julai 4 mwaka huu, Mongella wakati akiwaapisha wakuu wapya wa wilaya saba za mkoa huo, alimuagiza Marry Tesha, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana kuwatimua machinga kutoka katikati ya jiji hilo kabla ya Agosti mosi mwaka huu.

Mongella ambaye alizamilia kuwaondoa wafanyabiashara hao ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiondolewa na kurudi katikati ya Jiji, alidai wamekuwa wakipanga biashara zao hadi kwenye milango ya watu hivyo wanapaswa kuondoka.

Mabula akizungumza jana na wafanyabiashara machinga wakati akikabidhi vifaa mbalimbali vya usafi, amesema kumekuwepo na taarifa za kuwatimuwa machinga mjini bila kukaa chini na kufanya maridhiano.

Amesema kuwa, hatakubali kuona machinga hao wakiondolewa mjini bila kuwepo kwa maridhiano ya pande zote mbili kwa maana ya serikali na wafanyabiashara hao ili kuangalia namna watatengewa maeneo ambayo ni rafiki kwa shughuli zao.

“Nimekuja hapa na mambo mawili, kwanza ni kukabidhi hivi vifaa vya usafi lakini pili nimekuja kuwaambia kwamba, endeleeni kufanya biashara zenu.

“Mimi najuwa hakuna machinga anaekataa kuondoka katikati ya jiji ila lazima eneo mtalopelekwa liwe rafiki,” amesema Mabula.

Mabula ambaye hata hivyo hakumtaja jina mkuu huyo wa mkoa, lakini kauli yake ilionekana kumlenga RC Mongella huyo, huku akidai kwamba wakati wa uchaguzi wa 2015, alipata wakati mgumu kujinadi kwa wananchi kutokana na tuhuma za kuwaondoa machinga hao wakati akiwa meya wa jiji hilo.

Amesema kuwa, halmashauli ya Jiji hilo, inapaswa kuangalia ni namna gani ya kuwaondoa machinga hao na kwamba maeneo wanayotaka kuwapeleka ikiwemo Sina (Mabatini) na maduka tisa huduma ya usafirishaji haifiki kitendo ambacho sio cha kweli.

“Kuna maeneo mengi ya kuwapeleka ambayo ni rafiki kwenu, kuna pale Mirongo Community centre ambayo yanatakiwa yabomolewe ili kama ni kwenda huko ndo machinga wapelekwe na sio maeneo ambayo sio rafiki,” amesema Mabula huku machinga hao wakimshangilia.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani hapa, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo kufuatia kuagizwa na RC Mongella kuwatimua machinga hao, simu yake ya mkononi haikupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi maneno (SMS) hakuujibu.

Mabula wakati akiwa Meya wa Jiji hilo, alishiriki kwa kiasi kikubwa kuendesha oparesheni ya kuwaondoa machinga mjini, jambo ambalo lilimpa wakati mgumu katika kampeni za uchuguzi wa mwaka 2015 huku machinga na mamantile wakimtuhumu kuvunja vyombo vyao vya kupikia (sufuria).

error: Content is protected !!