Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Mbunge: Nguvu ya umma imezidi Mazombi
Makala & Uchambuzi

Mbunge: Nguvu ya umma imezidi Mazombi

Kundi la watu wenye kufunika uso Zanzibar (Mazombi)
Spread the love

KUFUMBA na kufumbua, Bwana Ali Juma Suleiman ametangulia mbele ya haki. La, bora niseme ametangulizwa mbele ya haki kwa kudhulumiwa na makundi ambayo yameshafanyia udhalimu mwingi wanachama wa chama kikuu cha upinzani nchini – The Civic United Front (CUF), anaandika Ally Saleh.

Marehemu Ali ameshafika na hesabu yake kwa Mola wake imeshaanza tokea Septemba 28, na wengi tunaamini amekufa shahidi kwa kuwa amedhulumiwa. Lakini pia amekufa shahidi kwa kuwa amekufa akipigania haki, usawa wa nchi jambo ambalo waliomuua hawalitaki kabisa.

Hata akiwa kitandani siku moja kabla ya kufariki aliendelea kusimama katika anachokiamini na alisema kuwa “Tusikubali kabisa kuonewa.” Na amini alikuwa akikariri Wimbo wa Taifa wa CUF ambao amekuwa akiuimba kwa miaka kadhaa tokea alipoingia chama ambacho wanachama wake wamepitia madhila mengi sana.

Marehemu Ali ameungana na wengine wengi waliouliwa kwa sababu tu ya imani zao za siasa ikiwa ni pamoja na waliokufa kimya kimya baada ya vifo kama hivi vya kupigwa toka zama za Janjaweed hadi sasa zama za Mazombie na wale ambao waliouliwa katika maandamano ya kudai haki yao katika tarehe 26 na 27 Januari 2001.

Wapo kwa makundi makubwa waliokufa kwa uonge na ukiwa baada ya dhuluma za kupigwa na kuteswa na kutiwa vilema, wako ambao wamebaki na vilema vyao wakichechemea na wengine wakiugua kisaklojia kutokana na yaliowakuta na kutwisha.

Yote haya ambapo, CUF imekusanya majina ya maelfu ya wahanga wa tokea Janjawidi hadi sasa Mazombie, vitendo vyengine vikifanywa mchana kweupe, na majina na ushahidi kupelekwa Serikalini ikiwa na pamoja na Bungeni, lakini hakuna lilokuwa.
Jeshi la Polisi halijawahi hata siku moja angalau kujaribu kuchukua hatua na wakibanwa wanasema wanaodhulumiwa wapekele ushahid. Kesi kwa maelfu ziko kwenye madaftari ya vituo vya Polis lakini hata moja haijafanyiwa uchuguzi.

Tumelisikia Jeshi la Polisi likikana kabisa kuwepo kwa Mazombie na kusema wao haiwajui, wala hawaamini kuwa wapo. Wananchi wamekuwa wakifanya kama ada tu kwenda vituo vya Polisi lakini wanajua kuwa Jeshi la Polisi halina uwezo wala nia ya kuwakamata watendaji hao wa maovu dhidi ya wenzao.

Binafasi nimekuwa nikilishikia bango suala hilo la Mazombie na hivi karibuni niliwasilisha majina ya wanachama na wapenzi wa CUF zaidi ya 350 ambao wameripoti matukio ya kupigwa, kuteswa na madhila mengine waliyofanyiwa, lakini hakuna kilichofanywa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba.

Mwigulu alitafuta suluhu kwa kutoa kauli wakati akitaka bajeti yake ipitishwe; baada ya (mimi) kuishika shilingi, lakini hadi leo hajanitafuta na wala sifikirii atanitafuta maana ni wazi kuwepo kwa Mazombi kunaungwa mkono na CCM na kuna maslahi na chama hicho.

Tulipopendekeza Bunge liunde kamati ya uchunguzi kuhusu jambo hilo, kwa kweli lilirahisishwa na kutupiliwa mbali kama mzigo uso na maana, na likazimwa kabisa.

Pamoja na yote yanayotokea, haijawahi kutokea Serikali ya Zanzibar wala Serikali ya Muungano kutoa kauli yoyote ya kulaani vitendo vya makundi hayo, ambavyo kuendelea kwake, kunadhihirisha kuwa nchi haina udhibiti na usalama. Basi SMZ na SMT wako radhi isemwe na ionekane hivyo kuliko kuchukua hatua zifaazo.

Pili, serikali kwa kukaa kimya ni sawa na kusema wako tayari isemwe kuwa inaridhia matendo hayo yafanywe kwa raia wengine ilhali ikijua wazi kuwa vitendo hivyo ni vya kibaguzi kwa vile vinalengwa watu maalum katika jamii kwa sababu ya imani zao za kisiasa.

Pia ni sawa na serikali kukiri kuwa vyama vingi haviko katika haki na mizania yake na kwamba kuwa CUF ni kosa, ni kupotea na hakuwezi kukubalika na ndio maana ya adabu, mateso, vipigo na dhulma zote.
Kwamba kijana mwenye nguvu zake na aliyeshiba maziwa ya mama yake wa CCM ana haki ya kumfanya lolote lile mwana CUF na hakuna litakalokuwa.
Hadhi waliyopewa Mazombi naweza kusema ni sawa na kundi la mgambo ambalo linaweza kufanya litakavyo na hakuna viwavyo. Ni ishara kuwa lipo juu ya sheria.

Nchi imefanya bidii zote kuzima vitendo vilivyokuwa vikifanywa Kibiti lakini kwa upande wa Zanzibar hakuna lilofanywa na zaidi wanakingwa na hata kukataa (denial) kuwa kundi au makundi hayo yapo.

Viongozi wa CUF kwa muda wote wamekuwa wakiwaambia wanachama wao wasichokozeke na wala wasirudishe mapigo wanayopigwa na huku wakijua kuwa wanachama wao wanajeruhiwa, wanatiwa vilema na kama hivyo wanauawa.

Jeshi la Polisi, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wamekuwa wakiwachukulia poa wanachama wa CUF na hivyo kuwapa kichwa Mazombi kuwa wanachofanya kina baraka zote zao na hakuna litakalokuwa.

Maziko ya Ali Juma Suleiman akisindikizwa na umati ambao haujawahi kutokea na ulimpeleka safari yake kwa miguu hadi makaburini, ni ishara kuwa CUF wanao watu wa kurudisha mapigo na hata kulipa kisasi na kama si hivyo, basi angalau kusimama kusema “kuanzia sasa basi.”

Tusiombee yule aonewaye kufika siku ya kusema palipofika basi, na siioni siku hiyo kuwa iko mbali tena. Naamini Mazombi hata kama wanaungwa mkono kama wanavyopewa nguvu, si wengi kuzidi umma wa CUF uliochoka na dhulma zao. Watu wamekuwa wakionewa toka 1992 kuliporudishwa vyama vingi kwa maana ya wapenzi wa mabadiliko, hapo pakiwa wakati CUF ilipoanzishwa. Mashtaka ya kubuni ili watu wawekwe selo au jela ni kwa maelfu mengi.

Ieleweke tu wanaochoka kuonewa wakijetetea basi Jeshi la Polisi ambalo haliwezi kuchukua hatua na Serikali ya Zanzibar na ile ya Muungano wanao nyamazia kimya, wasije kugeuza lawama kwa walioonewa angalau wakinyanyua mkono kujikinga au kurudisha kofi kwa kofi.

Tuombe tusifike huko lakini kutanzwa kukizidi kama inavyosukumwa na dola iwe, lolote laweza kuwa.
Mwandishi ni mbunge wa Mji Mkongwe, muandishi wa habari mwandamizi nchini aliyewahi kutangazia Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) na pia ni mwanasheria.
Ends.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!