August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge mwingine wa CCM, kizimbani kwa rushwa

Spread the love

RICHARD Mganga Ndassa, mbunge wa jimbo la Sumve (CCM), amepandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka la tuhuma ya kuomba rushwa ya Sh. 30 milioni, anaandika Faki Sosi.

Akisoma mashtaka hayo, mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Amilisi Mchaura, wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Denis Lukayo amesema, Ndassa alitenda kosa hilo akiwa mbunge wa Bunge la Muungano.

Amesema, mbunge huyo akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ya Bunge la Jamhuri, aliomba rushwa kwa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme la taifa (Tanesco), Felichesmi Mramba, ili amsaidie kuandika mapendekezo safi ya shirika lake.

Mbunge huyo wa miaka mingi katika jimbo la Sumve, mkoani Mwanza, alifikishwa mahakamani hapo majira ya saa mbili asubuhi, huku idadi kubwa ya watu wakiwa wamefurika kushuhudia kesi hiyo ambayo imekuwa na mvuto mkubwa kwa wananchi.

Mara baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili, mtuhumiwa alikana kutenda kosa hilo. Upande wa mashitaka umesema upelelezi bado wa shauri hilo, bado unaendelea. Mtuhumiwa yuko nje kwa dhamana.

Ndasa anakuwa mbunge wa nne kupandishwa kizimbani kwa kosa la kuomba rushwa. Jana wabunge wengi watatu walipandishwa kizimbani kwa makosa kama hayo.

Wabunge waliopandishwa kizimbani jana, ni pamoja na mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (54), mbunge wa Mvomero, Ahmad Saddiq (53) na mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa (63). Wote ni kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Taarifa zinasema, kuna uwezekano mkubwa wabunge wengine kadhaa, huenda wakafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo ambazo zimetikisa taasisi ya Bunge – chombo kikuu cha kutunga sheria nchini.

error: Content is protected !!