August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Mbunge’ Mtambile aaga dunia

Spread the love

KIONGOZI Mwandamizi wa Chama cha ACT Wazalendo na Mbunge wa zamani wa muda mrefu wa Mtambile, Masoud Abdalla Salim amefariki dunia leo. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea). 

Taarifa zilizotufikia kutoka Kisiwani Pemba, zinasema mauti yamemkutia akiwa amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba.

Maziko yake yalitarajiwa kufanyika laasiri leo Jumatatu kijijini kwao Jonza jimboni Mtambile.

Taarifa ya ACT Wazalendo iliyosainiwa na Salim Abdalla Bimani ambaye ni Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma, inasema marehemu amekuwa Msemaji wa Kisekta wa Chama, masuala ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) akikabidhiwa dhamana kwa uzoefu wake wa kuwa mbunge wa vipindi vitatu kufikia mwaka 2015 wakati akiwa Chama cha Wananchi (CUF). Marehemu anafahamika vilivyo kwa michango yake ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Marehemu hakuyumba wakati umma wa CUF ulipoelekezwa “kushusha tanga na kupandisha tanga” ili kuhamia ACT Wazalendo Agosti mwaka 2019.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kutamka kukihama chama hicho na kuhamia ACT Wazalendo na akataka watu wote waliokuwa wanamuamini wamfuate.

Marehemu Masoud aliunga mkono lakini pamoja na wabunge wenzake wakati ule, “kimkakati” walibakia kutumikia ubunge mpaka muda wa bunge ulipomalizika na kuingia uchaguzi wa 2020.

Alihamia ACT Wazalendo mara tu Bunge lilipovunjwa kuelekea kufanyika kwa uchaguzi mkuu. Na wakati ulipofika wa maandalizi ya uchaguzi 2020, aliomba kuteuliwa tena kugombea ubunge kupitia ACT Wazalendo. Hata hivyo alishindwa kwenye kura za maoni.

ACT Wazalendo imejipanga kushiriki kikamilifu kumzika na Mratibu wake kisiwani Pemba, Said Ali Mbarouk pamoja na mawaziri kutokea chama hicho Nassor Ahmed Mazrui na Omar Said Shaaban wataongoza umma kuwakilisha chama.

error: Content is protected !!