October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge Malleko ampongeza Rais Samia

Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Kilimanjaro, Esther Malleko

Spread the love

 

MBUNGE wa Viti Maalum, Mkoa wa Kilimanjaro, Esther Malleko amempongeza Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kufikisha mwaka mmoja madarakani kwa mafanikio lukuki. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).

Malleko amesema, Rais Samia katika utawala wake, amegusa maeneo yote ya sekta ya elimu, uboreshwaji wa huduma za afya, maji safi mijini na vijijini, uwezeshaji wananchi kiuchumi na uendelezaji wa sekta ya kilimo.

Mbunge huyo amesema hayo leo Ijumaa, tarehe 18 Machi 2022 alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari kuhusu mwaka mmoja wa Rais Samia tangu alipoingia madarakani 19 Machi 2021.

“Kama mnavyoelewa mambo mengi ya elimu kwa watoto, mama ndiye anaesimamia na kuyajua hivyo kuboresha sekta hii ni kumkomboa mwanamke na kumrahisishia mambo yake,” amesema

Amesema, Mkoa wa Kilimanjaro unaendelea na mikakati yake ikiwemo kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa watoto wetu.

Rais Samia Suluhu Hassan

“Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan imetufanyia makubwa kwenye sekta ya afya na kina mama wa Mkoa wa Kilimanjaro tunampongeza na kumuomba azidi kutuangalia kwa jicho la upekee,” amesema

Kuhusu huduma ya maji, Mbunge huyo amesema, “sote ni mashahidi kuwa sehemu yenye changamoto ya maji mtu pekee anaepata tabu kuyatafuta ni mwanamke ili yakahudumie familia yake hivyo kuboreshwa kwa sekta hii kumemuinua sana mwanamke wa Mkoa wa Kilimanjaro”.

Amesema, katika Mji wa Moshi huduma ya maji safi inapatikana katika mitaa yote hivyo maji yanapatikana kwa asilimia mia moja (100).

“Kwa upande wa Vijijini jumla ya vituo vya maji 354 vinavyotoa huduma ya Maji kwa Wananchi 170,974 katika vijiji 72 vimejengwa ambapo upatikanaji wa huduma ya Maji kwa sasa ni asilimia 83,” amesema

Mbunge Malleko amesema, kwenye eneo la uwezeshaji wananchi kiuchumi akigusia fedha zinazotolewa na halmashauri zetu za Mkoa wa Kilimanjaro kwa Wanawake, Vijana wetu na ndugu zetu watu wenye Ulemavu yaani ile asilimia 10 ambayo wanawake wanapata asilimia 4, Vijana asilimia 4 na Watu wenye Ulemavu asilimia 2.

Amesema, kwa kipindi cha Mwaka Mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan fedha zilizotolewa kama Mikopo ni Sh.903.4 milioni.

Amesema, Jumla ya vikundi vilivyonufaika ni 310 ambapo vikundi vya wanawake 164 vilikopeshwa kiasi cha Sh.383.04 milioni, vijana vikundi 97 vilikopeshwa kiasi cha Sh.379.44 milioni na watu wenye Ulemavu vikundi 49 vilikopeshwa Sh.140.9 milioni.

error: Content is protected !!