Wednesday , 29 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Mbunge Jesca Kishoa avunja ndoa na Kafulila
Habari za SiasaTangulizi

Mbunge Jesca Kishoa avunja ndoa na Kafulila

Wengine watatu nao tayari wamefanya hivyo, huku wawili ikiwa ‘tia maji tia maji’

Spread the love

 

NDOA baina ya Jesca David Kishoa, mbunge wa Viti Maalum katika Bunge la Jamhuri na David Kafulila, Kamishena katika wizara ya fedha, anayeshughulikia Ubia kati ya sekta ya binafsi na sekta ya umma (PPP), sasa imevunjika rasmi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Tangazo la kuvunjika kwa ndoa hiyo, iliyofungwa tarehe 24 Aprili 2014, limetolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Temeke, 20 Februari 2023.

Kwa mujibu wa Mahakama, uamuzi wa kuivunja ndoa na wanasiasa hao wawili, umetokana na Jesca kuieleza Mahakama, kuwa “ndoa baina yake na Kafulila, imevunjika kiasi cha kutokurekebeshika.”

Aidha, Jesca aliomba Mahakama kutoa amri ya kuvunja ndoa, kuishi na watoto na amri ya matunzo ya watoto dhidi ya Kafulila, ambaye katika shauri hilo Na. 2017 ya mwaka 2022, alitambulika kama mjibu maombi.

Hata hivyo, katika kile ambacho hakijaweza kufahamika wazi, Kafulila ambaye amepata kuwa mbunge wa Kigoma Kusini, kupitia NCCR- Mageuzi (2010 hadi 2015); katibu tawala wa mkoa wa Songwe na mkuu wa mkoa wa Simiyu, hakuwa na pingamizi dhidi ya maombi hayo.

Katika hili, Mahakama inasema, “…tarehe 4 Oktoba 2022, mjibu maombi aliwasilisha majibu yake. Hakuwa na pingamizi juu ya maombi yaliyowasilishwa mahakamani na Jesca.

“Eden Kitalu na Rashida Hussein, mawakili wasomi, wamemwakilisha mleta maombi na mjibu maombi, mtawalia. Kitalu ameiomba Mahakama kutoa hukumu kwa kuzingatia shauri la Joseph Warioba Butiku na Perucy Muganda Butiku (1987) TRL1.”

Hatua ya Jesca kuamua kuvunja ndoa yake aliyoifunga kabla ya kuwa mbunge, imekuja katika kipindi ambacho tayari wabunge wengine wanne wanawake wa Chadema, waliokuwa wamefunga ndoa kabla ya kushika wadhifa huo, tayari wamevunja ndoa zao, huku mwingine wa tano, ndoa yake ikiwa “tia maji.”

Waliovunja ndoa mpaka sasa, ni Kunti Majala, Suzana Masele na Grace Kihwelo. Wabunge wengine wawili ambao ndoa zao ziko mashakani, ni pamoja na Devota Minja na mwingine jina lake tunalihifadhi kwa sasa.

Devota Minja

Kupatikana kwa taarifa kuwa Jesca amewasilisha maombi mahakamani ya kuomba kuvunja ndoa baina yake na Kafulila, kumekuja wakati kumeibuka wimbi la wanawake wa Chadema, waliobahatika kupata ubunge, na Jesca hizi, kumekuja wakati kumeibuka taarifa.

Katika maamuzi yake ya kuvunja ndoa baina ya Jesca na Kafulila, Mahakama ya Hakimu Mkazi Temeke imesema, inakubaliana na hoja zilizotolewa na mleta maombi na imejiridhisha kuwa ndoa hiyo, haiwezi kurudi katika hali yake ya awali.

“Kwa upande wangu, sina mashaka kuwa ndoa ya wadaawa imevunjika kiasi cha kutokurekebishika chini ya kifungu 107 (2) (f) cha Sheria ya Ndoa. Kwa msingi huo, amri ya kuvunja ndoa na talaka inatolewa,” anaeleza Hakimu Mkuu Mkazi, Swai, S.O.

Kunti Majala

Anaongeza, “sambamba na hilo, watoto wataishi chini ya uangalizi wa mama yao. Mjibu maombi (Kafulila), atakuwa na haki ya kuwaona na kuwa na watoto wake, mwishoni mwa juma – kuanzia Ijumaa saa 12 jioni hadi saa 12 jioni ya Jumapili – pamoja na vipindi vya likizo.”

Mahakama inasema, chini ya kifungu 129 cha Sheria ya Ndoa, mjibu maombi anawajibika kutoa matunzo ya watoto kikamilifu.

“Ada zote za shule zitaendelea kulipwa kwa uwiano linganifu (asilimia 50) kwa kila mzazi katika shule watakazokubaliana pamoja; kutokana na asili ya shauri hili, hakuna amri ya gharama inayotolewa.”

Jesca David Kishoa, aliingia bungeni kwa mara ya kwanza, Novemba 2015, kufuatia kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katika uchaguzi mkuu uliyopita, Jesca aliungana na wanawake wengine 17 waliokuwa wanachama wa chama hicho, walitumika kukisaliti chama chao kwa kukubali kujipeleka bungeni kuapishwa kuwa wabunge, kinyume na maelezo ya chama chenyewe.

Suzana Masele

Wanawake hao, wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima Mdee, walituhumiwa na kupatikana na hatia kwenye makosa ya usaliti, kughushi nyaraka za chama, kujipeleka bungeni kuapishwa, kushirikiana na wanaokitakia mabaya chama, ubinafsi na uchonganishi.

Walifukuzwa uanachama wa Chadema na kikao cha Kamati Kuu (CC), kilichokutana tarehe 27 Novemba 2020. Wakati wote huu, Jesca alikuwa Naibu Katibu mkuu wa Bawacha.

Wanawake wote 19, wameendelea kuwa bungeni kutokana na kile Spika wa Bunge, Tulia Akson, ameweza kukiita, “kuwapo mahakamani shauri la kupinga kufukuzwa kwao.”

Grace Kihwelo

Wengine waliofukuzwa Chadema, pamoja na Mdee na Jesca, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega; aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara), Hawa Subira Mwaifunga na aliyekuwa katibu mwenezi, Agnesta Lambat.

Katika orodha hiyo, wamo pia aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed; aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.

Wengine waliofukuzwa Chadema, ni Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

TEMESA iliyokarabati Kivuko kwa Bil 7.5 yapata hati chafu

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yakusanya Mil 8.5/- kodi ya zuio na kutokomea nazo

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

DC Kasilda Mgeni ahamasisha chakula shuleni

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni...

Habari za Siasa

Bilioni 223.9 zapelekwa Tunduru ndani ya miaka 2 ya SSH

Spread the love  ZAIDI ya Sh. bilioni 223.9 zimepelekwa Wilaya ya Tunduru...

error: Content is protected !!