July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge, Diwani na Wenyeviti wapinga bomoa bomoa Dar

Spread the love

MBUNGE wa Jimbo la Kinondoni Maulid Mtulia, Diwani wa Kata ya Hananasifu pamoja na wenyeviti wa kata 13 zilizopo Kinondoni wamekwenda kwa mkuu wa Mkoa Meck Sadiki ili kuomba zoezi la ubomoaji wa nyumba mabondeni usitishwe. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Mtulia amesema wamepeleka maombi matatu ambayo ni vilio vya wananchi wengi.

Kati ya maombi ambayo waliyapeleka viongozi hao kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kinondoni ni pamoja na, kuiomba serikali ipitie upya mchakato wa ugawaji viwanja kwa wakazi wa mabondeni kwa maelezo kwamba baadhi ya wananchi wanadai wao hawakupata viwanja hivyo hawana pa kwenda.

Mtulia alisema pia  iache zoezi hilo kwani wananchi wanalalamika kuwa zoezi hilo limeshitukizwa japo lilitangazwa kwa muda mrefu, na kwamba walikuwa hawana sehemu ya kwenda kuanza makazi mapya. Hivyo mbunge huyo na viongozi wa serikali za mitaa wameiomba serikali kuwapatia wananchi siku saba za kujiandaa ndipo zoezi hilo liendelee.

Ombi lao la tatu ambalo wameiomba serikali ni kwamba, wananchi wengi wao hawana sehemu za kujihifadhi kwa sasa, hivyo serikali inatakiwa kuwatazama kwa jicho la tatu au kuwatafutia wafadhili ambao watakuwa wako tayari kuwasaidia hata kwa chakula, mavazi hata sehemu za kujihifadhi wakati huu ambao hawana mahali pa kwenda.

“Sawa hilo ni agizo la serikali lakini pia serikali inatakiwa kuwa na huruma kwa wananchi wake kwani wengi wao hawana makazi. Pia ingefaa wafanye uhakiki kwa wale ambao walipewa viwanja ndio wangekuwa wa kwaza kuvunjiwa na wale ambao hawakupewa wapate haki zao”

Akitolea majibu maombi hayo kwa niaba ya mkuu wa Mkoa Rymons Mushi amesema, “nimeyasikia maombi yao nimeyapokea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa na nitayafikisha kama yalivyo, peke yangu siwezi kutolea uamuzi kwa kuwa hili ni jambo ambalo linahusisha taasisi nyingi hivyo kesho tutakutana baada ya Mkuu wangu kurudi safarini. Jibu tutatoa kesho na kuwajulisha kama maombi yamekubalika”.

Mushi amedai kuwa, serikali inatumia nguvu kubwa kwa sasa kubomoa kuliko kuwaondoa wananchi kwa kuwa walishaambiwa mapema lakini waliendelea kukaidi na kuishi katika maeneo ambayo ni hatarishi.

Aidha,  amesema kuwa , serikali ipo tayari kuyapitia na kuhakiki waliopewa viwanja na kutakiwa kuondoka na wale ambao hawakupatiwa viwanja sheria itafuata mkondo wake kama wanahati miliki ya kiwanja chake atapatiwa haki yake. Hata hivyo, zoezi la ubomoaji utaendelea hadi pale serikali itakapokubali maombi yaliyopelekwa leo.

error: Content is protected !!