MBUNGE wa Viti Maalum (CCM), Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile amejumuika na viongozi wa Dini, Serikali, Chama Cha Mapinduzi na wananchi mbalimbali katika Dua maalum aliyoiandaa ya kuliombea Taifa na Rais Samia Suluhu Hassan. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Aidha, ameshiriki nao futari ya pamoja aliyoiandaa jana Jumatano tarehe 27 Aprili 2022 Dodoma.
Dua hiyo maalumu imefanyika katika viwanja vya Kitengo Bicha wilayani Kondoa kilipo kituo cha kulelea Watoto Yatima na wenye uhitaji.
Ditopile amewasihi Watanzania na wananchi kwa ujumla kumuombea Rais Samia kwani tangu ameingia madarakani ameonesha dhamira yake ya kuiletea maendeleo nchi yetu.

“Niwashukuru kwa kutenga muda wenu kukubali kushiriki Dua hii Maalum ya kuliombea Taifa letu na Rais wetu Samia Suluhu Hassan, ombi langu kwenu tuendelee kumuunga mkono kiongozi wetu ambaye hakika mambo aliyoyafanya ndani ya kipindi cha miezi 14 madarakani ni makubwa hivyo anahitaji kutiwa moyo,” alisema
“Niwaombe kuiunga mkono Serikali yenu ya awamu ya sita ambayo imeendelea kuongoza nchi yetu kwa amani na sisi leo tunafanya Dua hapa kukiwa na utulivu huku tukiendesha shughuli zetu za kiimani kwa amani na utulivu, ” alisema sema Ditopile.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania kushiriki kwa ukamilifu zoezi la Sensa ambalo linatarajiwa kufanyika tarehe 23 Agosti 2022 akisisitiza ushiriki wa wananchi utasaidia Serikali kujua idadi ya wananchi wake katika kupanga bajeti za kuwaletea maendeleo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Sheikh wa Mkoa wa Dodoma alimpongeza Mbunge Mariam kwa namna alivyojitoa kuandaa Dua hiyo maalum ya kuiombea Nchi na Rais Samia sambamba na kuandaa futari hiyo.
Alisema tangu Rais Samia aingie madarakani amefanya mambo makubwa ya kimaendeleo huku akizidi kuwaunganisha Watanzania bila kujali tofauti zao za kiimani na vyama.
“Rais Samia kwa kipindi kifupi amefanya kazi kubwa ya kimaendeleo, kutengeneza mahusiano na kutuunganisha kwa pamoja, sisi kama viongozi wa Dini tutaendelea kumuunga mkono, kumuombea ili azidi kuwa na afya njema na kuwatumikia watanzania.”
“Ni jambo kubwa na la kiimani kuandaa Dua Maalum ya kumuombea Rais Samia na Nchi yetu, nikupongeze sana Mhe Mariam Ditopile kwa upendo huu mkubwa na zaidi kutuandalia futari ya pamoja, hii inaonesha ukomavu wako kama Kiongozi na moyo wa Upendo ulionao,” alisema.
Leave a comment