May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge Chadema aibana Serikali bungeni

Aida Khenan, Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema)

Spread the love

 

AIDA Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amehoji lini Serikali itapeleka fedha jimboni humo, kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa vituo vya afya, ulioanzwa kutekelezwa na wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Khenani ameuliza swali hilo leo Jumatano tarehe 28 Aprili 2021, bungeni jijini Dodoma.

Mbunge huyo wa Chadema amesema, Jimbo la Nkasi Kaskazini lina uhaba wa vituo vya afya, ambapo kuna vituo viwili katika kata 17 za jimbo hilo.

“Katika kata 17 tuna vituo vya afya viwili tu, lakini kuna vituo vimeanzishwa kwa nguvu za wananchi. Lini serikali itapeleka fedha kwenye Kata ya Kabwe ili kuheshimu na kuendelea kuhamasisha wananchi kujitolea?” amehoji Khenani.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Dk. Festo Dugange, amesema katika mwaka ujao wa fedha 2021/22, Serikali imepanga kujenga vituo vya afya 108 na Zahanati 578, na kwamba katika mpango huo Nkasi Kaskazini itapewa kipaumbele.

Dk. Festo Dugange, Naibu Waziri (Tamisemi)

“Serikali inatambua na inathamini sana nguvu ya wananchi na tutaendelea kuhakikisha tunatenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma ambayo wananchi wameanza kuyajenga kwa nguvu zao. Mfano mzuri bajeti ya mwaka ujao maboma zaidi ya 108 kwa maana ya vituo vya afya vitakwenda kujengwa,” amesema Dk. Dugange na kuongeza:

“Lakini kuna zahanati 578 zitakwenda kujengwa, naomba nimhakikishie katika mpango huu ujao pia Jimbo la Nkasi Kaskazini tutalipa kipaumbele. Kuhakikisha kwamba wananchi wanaoana matunda ya serikali yao katika kujali nguvu walizoweka katika maboma yale.”

error: Content is protected !!