December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge CCM azichongea halmashauri bungeni

Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga

Spread the love

GOODLUCK Mlinga, Mbunge wa Ulanga kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), amezichongea halmashauri bungeni, kwamba zina tatizo kubwa la matumizi mabaya na ubadhirifu wa fedha za mapato. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mlinga ameibua tuhuma hizo wakati akiuliza swali bungeni jijini Dodoma, leo Ijumaa tarehe 12 Juni 2020. Katika swali lake, Mlinga amehoji Serikali imejipanga vipi kukabiliana na tatizo hilo.

“Kumekuwa na tatizo kubwa la matumizi mabaya na ubadhirifu wa fedha za mapato ya ndani pamoja na ruzuku katika Halmshauri nyingi nchini, je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na tatizo hili,” amehoji Mlinga.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, amesema Serikali imeboresha mfumo wa ukusanyaji mapato na matumizi, ili kukabiliana na tatizo hilo.

“Katika kukabiliana na ubadhilifu wa fedha kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo, kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato na mifumo ya matumizi (Epicor 10.02 na FFARS) ili kudhibiti ubadhilifu wakati wa makusanyo na wakati wa matumizi,” amesema.

Waziri huyo mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, amesema katika mwaka wa fedha wa 2018/2019, Serikali ilizipatia halmashauri zote nchini, mashine bora na za kisasa za kielektroniki kwa ajili ya kukusanya mapato.

Aidha, amesema Serikali  imeimarisha mfumo wa ukaguzi wa ndani kuanzia ngazi ya Halmashauri, pia inatoa ushirikiano wa kutosha kwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kumuwezesha kufanya kazi yake kikamilifu.

“Serikali pia imekuwa ikichukua hatua za kinidhamu na kisheria kwa watumishi wote wanaobainika kuhusika kwenye ubadhilifu wa fedha za Umma,” amesema Waziri wa Tamisemi.

error: Content is protected !!