April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge CCM atetea wafungwa wajawazito

Spread the love

MBUNGE Viti Maalum (CCM), Angelina Malembeka ameishauri serikali kuweka utaratibu kwa wafungwa wa kike wenye ujauzito, kupewa vifungo vya nje ya gereza, ili watoto wao wazaliwe kwenye familia huru. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Malembeka ametoa hoja hiyo leo tarehe 17 Aprili 2019 bungeni jijini Dodoma, akihoji kwamba serikali inazingatiaje haki za watoto wanaozaliwa gerezani pindi mama zao wanapotumikia vifungo vyao. 

“Je, serikali ina wasaidiaje watoto ambao wako gerezani na mama zao, kieleimu na kisaikolojia kwa kuzingatia haki za watoto hususan wanapotumikia kifungo hicho ambacho watoto hao hawahusiki.

“Je, serikali haioni umuhimu sasa wa wanawake wafungwa ambao ni wajawazito wakatumikie kifuko nje  ili waweze kuwalea watoto wao katika familia huru badala ya gerezani?” amehoji.

Akijibu swali la Malembeka, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema, Jeshi la Magereza lina utaratibu wa kuwalea watoto hao kisaikolojia ili wasijione kama wafungwa na kwamba, wakifika umri wa kuishi bila ya malezi ya mama zao, hukabidhiwa kwa ndugu wa mfungwa husika ili akalelewe uraiani.

“Ni kweli kwamba, wako wakina mama wafungwa ambao wanajifungua watoto wakiwa gerezani, nataka nimhakikishie utaratibu wa Jeshi la Magereza kupitia kanuni za magereza, tunao utaratibu kwamba watoto wakishazaliwa magerezani wakifikia umri wa kusoma shule za awali husoma katika shule za awali zilimo katika magereza yetu,” amesema na kuongeza Lugola.

“Lakini pia kwa kupitia watumishi wa magereza ambao wana utaalamu wa masuala ya ustawi wa jamii,  wamekuwa wakiwapa elimu na kuwafariji watoto hao ili wajione sio wafungwa katika magereza bali walizaliwa katika wakati ambao mama zao wako magerezani.”

Aidha, amesema Jeshi la Magereza lina utaratibu wa kuwapa vifungo vya nje kina mama wajawazito ambao vifungo vyao ni chini ya miezi mitatu.

“Tumekuwa tukiandaa utaratbu na mchakato, wale wenye vifungo chini ya miezi mitatu wa kuwaondoa magerezani ili wapatiwe vifungo mbadala, lakini hata hivyo kuna utaratibu watoto wanao kuwa magerezani wakifikia umri wa kuishi uraiani bila ya kuwa na mama zao. Ndugu wamekuwa wakishirikishwa ili watoe malezi kwa watoto ambao mama zao wako gerezani,” amesema Lugola.

Naye Mbunge wa Konde, Khatib Haji amedai kwamba kuna taarifa za baadhi ya wafungwa wa kike kupata ujauzito wakiwa gerezani, huku akihoji inakuwaje wafungwa hao wanapata ujauzito wakati wanalingwa na walinzi wa kike.

“Zipo taarifa kwamba wako baadhi ya wanawake wanaoingia si wajawazito lakini wakapata ujauzito ndani ya magereza, na inaeleweka walinzi wa wafungwa wa kike ni wanawake. Mimba hizi wanazipataje mheshimiwa  waziri?”amehoji Haji.

Akijibu swali la Haji, Lugola amekanusha madai hayo akisema kwamba hakuna mfungwa wa kike anayepata ujauzito gerezani, huku akikisitiza kwamba sheria haziruhusu wafungwa wa kike kukutana kimwili na wenza wao pindi wanapotumikia vifungo vyao.

“Hakuna mimba ambazo zinatokea magerezani hilo la kwanza, lakini la pili mimba tunazozungumzia ni zile ambazo mfungwa mahabusu anaingia gerezani akiwa tayari kule uraiani anakotoka anapata ujauzito,” amesema na kuongeza Lugola

“Ndio maana kulitokea jaribio hapo kwa wabaunge wakitaka iwekwe sheria au utaratibu wa kuruhusu wenza wa wafungwa wakiwa gereza wapate fursa ya kufunguka wakiwa gerezani , wapate fursa wakajinafasi gerezani, lakini tulisema kwamba kwa sheria zetu na mila zetu hatuwezi kuruhusu hali hiyo.”

error: Content is protected !!