Spread the love

 

MBUNGE Viti Maalumu (CCM), Neema Lugangira, ameshauri Sheria ya Vyama vya Siasa irekebishwe ili kumpa meno Msajili wa Vyama vya Siasa katika kuvisimamia vyama kwenye utekelezaji wa usawa wa kijinsia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Lugangira ametoa ushauri huo leo Alhamisi, tarehe 28 Aprili 2022, akichangia makadirio ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria, kwa mwaka wa fedha wa 2022/23, bungeni jijini Dodoma,

“Serikali ilete Sheria ya Vyama vya Siasa ifanyiwe maboresho ili Msajili wa Vyama vya Siasa aweze kuwa na meno ya kuvisimamia vyama vyenyewe kutekeleza na kuimarisha usawa wa kijinsia kwenye siasa,” amesema Lugangira.

Lugangira ametoa ushauri huo akidai, sheria ya sasa haimpi Msajili wa Vyama vya Siasa meno ya kuvilazimisha vyama kutekeleza suala hilo.

“Pamoja na kwamba sheria imeweka mazingira wezeshi, bado matakwa haya yanakuwa magumu kutekelezeka sababu yanamfanya msajili anakosa meno ya kuvilazimisha vyama vitekeleze usawa wa kijinsia,” amesema Lugangira.

Katika hatua nyingine, Lugangira ameiomba Serikali ifanye marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi, ili kuweka adhabu kwa watu wanaofanya ukatili wa kijinsia kwa wanawake wanaogombea, wakati wa kampeni za uchaguzi na baada ya mchakato huo kumalizika.

“Hii ni pamoja na Sheria ya Uchaguzi iweke wazi pale ambapo mgombea mwanamke katika mchakato wa kampeni anapofanyiwa ukatili wa kijinsia, ikiwemo mtandaoni, ieleze hatua gani zinachukuliwa,” amesema Lugangira.

Jaji Francis Mutungi

Naye Mbunge Viti Maalumu asiyekuwa na chama bungeni, Salome Makamba, ameshauri mabadiliko ya sheria hiyo yaelekeze mtu anayekutwa na hatia ya kumfanyia mgombea mwanamke ukatili wa kijinsia aenguliwa kugombea wakati wa uchaguzi.

“Napenda kumpa taarifa, Sheria ya Uchaguzi inataka unapofanyiwa makosa yoyote ya kimaadili kama ni la kijinai, unatakiwa upeleke kwenye mfumo wa kijinai,” amesema Makamba na kuongeza:

“Sheria ieleze wazi kama imetokea kosa la jinai aliyefanya apewe adhabu kupitia kamati ya maadili ambayo inasimamia uchaguzi na moja ya adhabu iwe mtu huyo kuenguliwa kwenye uchaguzi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *