September 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge CCM ataka polisi waongezewe posho, Waziri amjibu

Simon Sirro, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP)

Spread the love

ANGELINA Malembeka, Mbunge Viti Maalumu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ameishauri Serikali iwaongezee posho askari polisi, ili wajiepushe na tamaa wanaposimamia zoezi la uchaguzi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Malembeka ametoa ushauri huo leo Jumanne tarehe 19 Mei 2020,  wakati akihoji mpango wa serikali katika kuwaongezea posho askari polisi, wanapotumiwa kulinda usalama kwenye vituo vya kupigia kura.

Katika swali lake kwa wizara ya mambo ya ndani, Malembeka amehoji sababu za askari polisi kutoka visiwani Zanzibar, kulipwa posho kidogo wanaposimamia zoezi la uchaguzi, ikilinganishwa na kiasi cha posho wanacholipwa askari polisi wa Tanzania.

“Je ni kwa nini askari waliopo Zanzibar hulipwa posho kidogo katika zoezi la uchaguzi tofauti na askari wa Tanzania Bara. Zanzibar hufanya chaguzi mbili zinazosimamiwa na mamlaka mbili, kwa nini wasilipwe posho mara mbili?” amehoji Malembeka.

Akijibu maswali hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani, amesema posho za askari polisi wakati wa chaguzi hupanga na kulipwa na mamlaka za chaguzi husika, na kwamba Jeshi la Polisi halihusiki.

“Kazi ya msingi ya askari polisi ni kuimarisha hali ya ulinzi na usalama, hivyo posho anayopata ni kwa ajili ya kujikimu anapokuwepo katika eneo la kazi,” amejibu waziri

Hata hivyo, waziri huyo amesema, Serikali inajitahidi kuboresha posho za askari polisi, kadri hali ya uchumi inavyoimarika.

“Mathalani, mwaka 2014/2015 Serikali ilipandisha posho ya askari toka Sh. 150,000 hadi Sh. 180,000. Kwa mwaka 2015/2016 Serikali ilipandisha posho hadi kufikia Sh. 300,000, ili kupunguza ushawishi wa aina yoyote,” amesema Simbachawene.

Nchi ya Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi Mkuu wa urais, wabunge na madiwani tarehe 25 Oktoba 2020.

error: Content is protected !!