September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge CCM amshambulia mteule Magufuli

Spread the love

MVUTANO kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali dhidi ya wafanyabiashara wadogo (Machinga) katika Jji la Mwanza unakita mizizi, anaandika Moses Mseti.

Stanslaus Mabula, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana (CCM) jijini humo amemshambuliwa mteule wa Rais John Magufuli, John Mongella ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwamba ni mkurupukaji.

Amesema Mongella anakurupuka katika kufanya uamzi wa hatua za kutaka kuwaondoa Machinga bila kufanyika maridhiano.

Tarehe 4 Julai mwaka huu, Mongella wakati akiwaapisha wakuu wapya wa wilaya saba za mkoa huo, alimuagiza Marry Tesha, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana na Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza kuwatimua machinga kutoka katikati ya jiji hilo.

Hata hivyo, tarehe 28 Julai mwaka huu katika kikao cha pili cha bodi ya barabara cha mwaka wa fedha wa 2016/ 17 kuliibuka mvutano mkali kati ya wabunge wa CCM mkoani humo na Mongella, kuhusu kuwatimua machinga hao na kutoa wiki mbili kufanya mazungumzo.

Mongella katika kuonesha amedhamiria kuwaondoa machinga hao ambao kwa kipindi kirefu kumekuwapo mvutano huo, anadai kuwa wafanyabiashara hao, wamekuwa wakipanga biashara zao hadi kwenye milango ya watu hivyo wanapaswa kuondoka.

Mabula akizungumza jana kwenye viwanja vya Liberty katika Kata na Wilaya ya Nyamagana jijini humo, wakati wa Mwenge wa Uhuru amesema kuwa, anashangaa Mongella kutaka kuwaonda machinga hao kwani wanapotaka kupelekwa hakuna huduma yoyote.

Amesema kuwa, Serikali ya Rais John Magufuli inajinasibu kuwasaidia wanyonge na kwamba, hatakubali kuona machinga hao wakiondolewa mjini bila kuwepo kwa maridhiano hayo.

“Sipingani na serikali yangu ila napingana na maamzi yasiokuwa na tija kwa wanyonge na nitaendelea kupingana na kiongozi wangu wa mkoa (John Mongella) kuhusu kuwaondoa machinga bila kukaa nao na kufanya maridhiano.

“Mimi niwaambie kwamba, nitakuwa mbele na nyie mtakuwa nyuma yangu katika kudai na kuoneshwa maeneo ambayo ni rafiki ya kufanyia biashara na hiyo ni baada ya kuyaona na kuridhika nayo kama yanatufaa,” amesema Mabula na kuongeza;

“Kuna maeneo mengi ya kuwapeleka ambayo ni rafiki kwenu, kuna pale Mirongo Community centre ambayo yanatakiwa yabomolewe ili kama ni kwenda huko ndo machinga wapelekwe na sio maeneo ambayo sio hata bajaji haifiki huko,” amesema Mabula.

Mabula pindi akiwa Meya wa Jiji hilo, alishiriki kwa kiasi kikubwa kuendesha oparesheni ya kuwaondoa machinga mjini, jambo ambalo lilimpa wakati mgumu katika kampeni za uchuguzi wa mwaka 2015.

 

error: Content is protected !!