September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge CCM amkaribisha Waziri Mpango ulingoni, asema…

Albert Obama, Mbunge wa Buhigwe

Spread the love

ALBERT Obama, Mbunge wa Buhigwe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma, amemjibu Dk. Phillip Mpango, Waziri wa Fedha, kufuatia kauli yake ya kutaka kuligombea jimbo hilo, kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Obama amesema, mwaka 2020 “Magufuli hapa, Obama hapa” kwani wananchi wa Buhigwe wanajua walipotoka, walipo na wanapokwenda hivyo hana wasiwasi na Dk. Mpango.

Jana Alhamisi tarehe 11 Juni 2020, Dk. Mpango alitangaza ‘kiana’ kugombea jimbo hilo, kupitia CCM, baada ya kuwataka wananchi wa jimbo hilo, kutomsahau kwenye harakati za uchaguzi ujao.

Waziri huyo, alitangaza nia hiyo wakati akihitimisha kuwasilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/21 ya Sh. 34. 87 trilioni.

Dk. Mpango ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, aliwataka wananchi wa Buhigwe pamoja na Watanzania kwa ujumla kumpatia Rais John Magufuli wabunge na madiwani wenye maadili watakaoenda sambamba na kauli mbiu ya hapa kazi tu, akiwemo na yeye.

Leo Ijumaa tarehe 12 Juni 2020 bungeni jijini Dodoma, Obama akichangia bajeti hiyo amesema yeye ni mashine ya Jimbo la Buhigwe, hivyo katika Uchaguzi huo, atapitishwa tena na CCM kugombea.

Dk. Philip Mpango, Waziri wa Fedha

Obama amesema, wananchi wa Buhigwe wanajua alipo watoa na atakapowapeleka, kutokana na utendaji wake katika kutatua changamoto zao, ikiwemo katika huduma ya afya, maji na elimu tangu mwaka 2010 alipochaguliwa kwa mara ya kwanza.

“Ukija kwenye orodha ya majina yangu bungeni utaambiwa, Obama anaitwa nani, utaambiwa ni mashine ya jimbo, mashine ya kusaga na kukoboa,  jina la nne utakaloambiwa kwangu ni simba wa yuda la mwisho ukiambwia ni katapila, “ amesema Obama huku shangwe zikiibuka bungeni

“Naomba hayo majina yawe katika hansard (taarifa) ya Bunge, Buhigwe wanajua tulikotoka, tuliko na tunakoelekea, niseme 2020 Magufuli hapa Obama hapa.”

Hata hivyo, Obama amempongeza Dk. Mpango kufuatia dua yake kuwataka wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti kupita bila kupingwa, ambapo yeye ni mmoja wapo.

“Nimpongeze Dk. Mpango amesema hivi anatuombea wajumbe wa kamati ya bajeti wapite kwa kishindo, kwa hiyo nakushukuru sana, umesema vizuri na mimi niko katika kamati hiyo tupite bila kupingwa,” amesema.

Wakati huo huo, Obama amelalamikia kitendo cha baadhi ya watu kumchafua mitandaoni, kwamba anatuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma.

“Spika kabla ya kwenda mbali naomba niseme jambo moja, wiki hii moja iliyopita kulikuwa na ‘clip’ (kipande za video) moja ilisema Takukuru inanichunguza mimi niliona kwenye mtandao, naomba kusema kwa kifupi na nichukue nafasi hii kumshuku mkurugenzi wa Takukuru, John Mbungo kwa kusema Obama yuko safi,” amesema Obama na kuongeza:

“Kulikuwa kuna watu wananihofu kwa kutumia vyombo wakafikiri nitachafuka Obama nina maadili niko safi kabisa,” amesema.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI ONLINE & MwanaHALISI TV ili kupata habari kemkem

error: Content is protected !!