August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge CCM amhofia JPM

Dk. John Pombe Magufuli, Rais wa Tanzania

Spread the love

BONEVETURA Kiswaga, Mbunge wa Magu mkoani Mwanza (CCM) ameonesha hofu katika utawala wa Rais John Magufuli kutokana na taifa kunyemelewa na njaa, anaandika Moses Mseti.

Amesema kuwa, janga la njaa linaloonekana kushamiri nchini, litasababisha utawala wa Rais Magufuli kuwa mgumu.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa Kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Mwanza (RCC) kilichokuwa kikijadili mambo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara na tatizo la maji.

Kiswaga amesema janga la njaa linaloonekana kuongezeka kwa kasi kubwa nchini hususan mkoani Mwanza, litasababisha wakati mgumu katika kuongoza watu kutokana na walio wengi kukabiliwa na njaa.

Amesema kuwa, viongozi wa mkoa huo hususani John Mongella, mkuu wa mkoa huo anapaswa kuacha kuoogopa kuomba chakula kutoka serikalini kwa kuwa hali ya chakula katika mkoa huo ni tete.

“Mnaogopa kuomba chakula kutoka ghala la serikali, kama tatizo ni uoga ni bora serikali ikauza chakula kwa wafanyabiashara na wao wakiuze chakula kwa wananchi kwa bei nafuu, hivi sasa guni moja la mahindi linauzwa Sh. 95,000 hadi Sh. 100, 000.

“Hali ni mbaya sana, ni ngumu kuongoza watu wenye njaa na hivi sasa kila kona ukipita ni tatizo lao kubwa ni njaa.

“Mvua isiponyesha wiki hii ama inayokuja sidhani kama watu watavuna chakula kwa sababu mazao yao yameharibika,” amesema Kiswaga.

Amesema tatizo la njaa linaweza kusababisha wanafunzi watapofungua, washindwe kusoma na wengine wataishia kunywa maji majumbani mwao na kurudi shuleni “Serikali Kuu inapaswa kuangalia suala hili.”

Kiswaga amesema kuwa, tatizo la njaa linalokabili mkoa huo sio la mtu mmoja, bali kila mmoja anapaswa kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi kuliko kuiachia serikali yenyewe.

William Ngeleja, Mbunge wa Sengerema ameiunga hoja hiyo na kudai kuwa, katika kipindi hiki taifa litakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula hivyo wafanyabiashara wanapaswa kuruhusiwa kuleta chakula kutoka ghara la serikali.

Pia Mongella amesema kuwa, suala la njaa wanalifahamu na kwamba, wanaendelea na jitihada za kuhakisha tatizo hilo halitaongezeka kwa kasi.

Soko kuu Mwanza

Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na mtandao huu wamesema, wanalazimika kuuza guni moja la mahindi Sh. 95,000 hadi Sh. 100, 000 kutokana na bei wanayonunulia kutoka kwa wakulima kuwa kubwa.

Wamesema kuwa, hivi sasa baadhi ya wafanyabiashara wamelazimika kusaga mahindi na kuuza unga kwa kilogramu kutokana na wateja (Wananchi) wengi kushindwa kumudu bei ya gunia la mahindi.

“Bei ya chakula sasa hivi ni kubwa sana, sio kwa sababu ya hizi sikukuu hapana, tatizo ni ukame huu, mvua hakuna na bei ya chakula imependa na sisi ni wafanyabiashara ni lazima tupate faida,” amesema Elias Buhenga.

error: Content is protected !!