May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge CCM aliyenusurika kifo kwa ajali, afariki kwa ajali

Mhandisi Atashasta Nditiye

Spread the love

 

MBUNGE wa Muhambwe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Atashasta Nditiye, amefariki dunia leo asubuhi Ijumaa tarehe 12 Februari jijini Dodoma. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Akitoa taarifa za kifo hicho bungeni jijini Dodoma, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema, Nditiye alipata ajali ya gari tarehe 10 Februari 2021, eneo la naenane alipokuwa amewapeleka wageni wake katika stendi ya mabasi ya Job Ndugai.

Amesema, baada ya kutokea kwa ajali hiyo, Nditiye aliyezaliwa tarehe 17 Oktoba 1969, alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma kwa matibabu hadi mauti yalipomfika leo Ijumaa saa 4 asubuhi.

“Kwa masikitiko makubwa, nawatangazia mwenzetu Mhandisi Atashasta Nditiye, amefariki dunia leo saa 4:00 asubuhi Hospitali ya Benjamin Mkapa,” amesema Spika Ndugai huku akiahirisha shughuli za Bunge hadi kesho Jumamosi

Spika Ndugai amesema, taarifa zaidi ya nini kinaendelea itatolewa huku akiwaomba wajumbe wa Kamati ya Uongozi kukutana.

Nditiye aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2015, alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, baada ya Rais John Magufuli kumteua, lakini kwenye baraza la sasa la mawaziri, hakurejea.

Anakuwa mbunge wa pili wa Bunge hili la 12 kufariki dunia, akitanguliwa na Martha Umbulla wa Viti Maalum (CCM), aliyefariki tarehe 21 Januari 2021 nchini India alikokuwa amepelekwa kwa matibabu.

Nditiye amefikwa na mauti kutokana na ajali ikiwa ni siku 824 kupita, tangu alipopata ajali tarehe 11 Novemba 2018 akiwa naibu waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano eneo la Iguguno mkoani Singida.

Katika ajali hiyo, hakuna mtu aliyejeruhiwa.

error: Content is protected !!