Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mbunge CCM alitishia gazeti la Raia Mwema, siri zaidi zafumuka
Habari za SiasaTangulizi

Mbunge CCM alitishia gazeti la Raia Mwema, siri zaidi zafumuka

Timotheo Paul Mzava, mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM)
Spread the love

 

TIMOTHEO Paul Mzava, mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), amelitishia gazeti la Raia Mwema, kuwa atalifikisha mahakamani kwa madai ya kuchapisha “habari za kashfa dhidi yake.” Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).

Kinachoitwa habari za kashfa, ni taarifa kuwa Mzava, anatuhumiwa kutelekeza mtoto na mama yake, anayefahamika kwa jina la Anna, ambaye walikuwa wakiishi nyumba moja mjini Dodoma, kama mke na mume.

Kwa mujibu wa tarifa zilizopo, uhusiano wa kinyumba kati ya Anna na Mzava, ulidumu kwa zaidi ya miaka mitatu, na kwamba wawili hao, wamefanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike, mwenye umri wa miezi saba.

Mgogoro kati ya Mzava na Anna, umeibuka kufuatia hatua ya mbunge huyo, kupata “chungu kipya” na hivyo kuamua kufunga ndoa na Caroline Pallangyo, mtoto wa mbunge wa Arumeru Mashariki (CCM), John Pallangyo, “bila kulipa fedha anazodaiwa,” na “kuhamishia kwenye miliki ya mtoto mali walizochuma.”

Aidha, taarifa ambazo Mzava anadai kuwa zinamchafua, ni zile zinazowanukuu mawakili wa Anna – Fred Kalonga, kutoka kampuni ya uwakili ya Heaven Lav Attorneys – kuwa wameelekezwa na mteja wao, kumburuza mahakamani mbunge huyo.

Anna amefikia maamuzi hayo, baada ya uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Usharika wa Mombo, mkoani Tanga, kulipa “kisogo pingamizi la ndoa aliloweka kati ya Mzava na Caroline.”

Vilevile, Anna ameamua kumburuza mahakamani Mzava, kufuatia mbunge huyo, kugoma kumtambua mtoto, kushindwa kumhudumia tangu alipozaliwa na “kukimbia madeni anayodaiwa na mzazi mwenzake.”

Kwa mujibu wa barua iliyotumwa na Lucky Mgimba, wakili kutoka kampuni ya mawakili ya Godwin Attorneys, tarehe 1 Julai 2021, Mzava anataka gazeti la Raia Mwema, kumuomba radhi ndani ya siku saba, tangu kupokelewa kwa barua yake.

Anasema, iwapo gazeti hilo litashindwa kufanya hivyo ndani ya kipindi hicho, ameelekezwa kufungua shauri la madai mahakamani.

Anataja habari nyingine anayosema kuwa ni uongo, ni ile iliyotolewa tarehe 28 Juni mwaka huu yenye kichwa cha maneno kisemacho: “Ndoa ya Mbunge, mtoto wa mbunge, yaingia mdudu.”

Wakili Mgimba anataja maneno yaliyomo kwenye gazeti hilo na ambayo anadai kuwa ni uongo, ni pamoja na “…ni kweli nimekuwa nikiishi na Mzava nyumba moja kama mume na mke hapa Dodoma, lakini miezi miwili baada ya mtoto kuzaliwa, nilikutana na picha mtandaoni ikionesha akimvisha pete mwanamke mwingine.”

Mengine ambayo anasema kuwa ni uongo, ni madai ya Anna kuwa amelitaarifu kanisa kuwa kuna mgogoro unaoendelea kati yake na Mzava, ambao unahusisha mtoto na mali walizochuma pamoja.

Wakili wa Mzava anasema, mteja wake analalamikia maneno kuwa “pale nyumbani kuna vitu vyake, kuna nyaraka zake muhimu bado,” kwamba habari hiyo haina ukweli na imetumika kumchafua mteja wake ambaye ni mbunge anayewakilisha wananchi.”

Anasema, “mteja wetu amechukua hatua hiyo ya madai kwa kuegemea mambo mawili makubwa ambayo ni habari kuwa sio ya kweli na imeegemea kwa kuhoji upande mmoja wa Anna.”

Pingamizi la ndoa kati ya Mzava na Caroline, liliwekwa na Anna, mwishoni mwa Juni mwaka huu. Ndoa kati ya Mzava na mchumba wake mpya, imepangwa kufanyika tarehe 10 Julai 2021.

Barua ya pingamizi iliwasilishwa na Anna mwenyewe na ilipokelewa katika kanisa hilo, Usharika wa Mombo, tarehe 26 Juni 2021.

Anna anasema, mara baada ya barua yake kupokelewa, aliahidiwa kuwa suala lake litashughulikiwa kabla ndoa haijafungwa, lakini mpaka sasa, hakuna kilichotekelezwa.

Wakati Mzava anadai gazeti la Raia Mwema, linamchafua, nyaraka zilizopo mikononi mwa Raia Mwema zinaonyesha kuwa “sakata” kati ya Anna na mbunge huyo, limefikishwa hadi kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Kwa mujibu wa Anna mwenyewe, ni kwamba baada ya kugundua Mzava ameanzisha uhusiano na mwanamke mwingine kwa kificho, huku akigoma kupokea simu yake, na kumtumia jumbe za vitisho, aliamua kutinga kwa Spika Ndugai, ili kumuomba aingilie kati jambo hilo.

Anasema, alikwenda kwa Spika Ndugai, ili aweze kupata haki yake, ikiwamo fedha anazomdai Mzava, zinazokaribia takribani Sh. 40 milioni.

Mara baada ya kukutana na Spika Ndugai na kumueleza mlalamiko yake, kiongozi huyo wa mhimili wa dola, alimtaka Anna kuwasilisha malalamiko yake kwa barua. Anna alifanya hivyo.

Mbali na kutaka Spika aingilie kati suala hilo, Anna alimtaarifu kupokea vitisho kutoka kwa mbunge wake, kupitia jumbe za simu ya mkononi (sms), na kwamba lolote litakalotokea litakuwa limefanywa na Mzava.

Anasema, mara baada ya Spika Ndugai kupokea malalamiko hayo, alimuagiza mmoja wa wasaidizi wake (jina tunalo), kulishughulikia suala hilo, kwa maelezo kuwa linachafua taswira ya mbunge husika na Bunge lenyewe.

Mzava aliitwa na msaidizi huyo wa Spika na kuelezwa kuwapo kwa malalamiko ya Anna na kwamba mbele ya afisa huyo, aliahidi kutekeleza madai yote yaliyowasilishwa mbele ya Spika.

Miongoni mwa yale ambayo Mzava alikubali kutekeleza, ni pamoja na kuwajibika kwa mtoto aliyezaliwa, kulipa fedha anazodaiwa na kurejesha mikononi mwa mtoto, baadhi ya mali walizoweza kuzimilikiwa wakati wakiwa wanaishi pamoja.

Hata hivyo, Mzava ambaye aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2018, baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Steven Ngonyani maarufu Prof. Maji Marefu, aliweza kulipa kiasi cha Sh. 5 milioni pekee kutoka kwenye fedha anazodaiwa.

“Baada ya hapo, Mzava hakuweza kupokea tena simu yangu na hakutaka kuwasiliana tena na mimi,” ameeleza Anna na kuongeza, “jambo ambalo limenilazimisha kuendelea kupigania haki yangu na mwanangu.”

Anna anaeleza kuwa baada ya kushindwa kwa ofisi ya Spika kumsaidia kupata haki zake zilizosalia, aliwasilisha malalamiko yake kwenye ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mjini Dodoma.

Haikuweza kufahamika mara moja, hatua ambazo ofisi ya katibu mkuu wa CCM ilichukua kuhakikisha haki za Anna zinapatikana.

Anna anadai kuwapo hati za viwanja ambazo zinahitaji kufanyiwa uhamisho, kama walivyokubaliana na Mzava, jambo ambalo halitaweza kufanyika ikiwa ndoa itafungwa kabla ya uhamishoni kwa kuwa kutahitajika ridhaa ya mke wake.

Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania

Gazeti hili, limefanikiwa kupata barua ambazo Anna ameziwasilisha kwa Spika Ndugai na kwa katibu mkuu wa CCM, zinazongumzia madai hayo, pamoja na akaunti ya benki ya NMB, iliyofunguliwa kwenye tawi la Bunge, mjini Dodoma.

Katika akaunti hiyo, iliyofunguliwa na Mzava mwenyewe, kiasi cha mwisho cha fedha kilichowekwa ni Sh. 98,000 (elfu tisini na nane elfu tu). Akaunti hiyo imeandikwa jina la mtoto (ambalo tunalihifadhi) na inasimamiwa na mbunge huyo.

Raia Mwema limefanikiwa pia kupata hati ya mashtaka yaliyofunguliwa kwenye Mahakama ya Watoto mjini Dodoma dhidi ya Mzava; na barua ya pingamizi la ndoa yake na mchumba wake mpya, iliyowasilishwa kwa Mchungaji wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Usharika wa Mombo, mkoani Tanga.

Gazeti hilo, limefanikiwa kunasa pia ujumbe uliyoandikwa na Mchungaji wa KKKT, Dayosisi ya Meru, Usharika wa Patandi, mkoani Arusha, anayejulikana kwa majina ya Franael Joshua Issangya, akieleza kumfahamu Mzava na Anna kwamba walikuwa wakiishi pamoja kama mke na mume.

Mchungaji Issangya ambaye ni swahiba wa karibu wa John Pallangyo, baba mkwe wa Mzava, ndiye aliyekuwa wa kwanza kukabidhiwa jukumu la kusimamia kile kinachoitwa, “makubaliano kati ya mbunge huyo na Anna,” ambayo nayo “hayakutekelezwa.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Chadema: Samia aunde tume kuchunguza mauaji mgodi wa Barick

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameombwa aunde tume huru kwa...

KimataifaTangulizi

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the love  TUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

error: Content is protected !!