April 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge CCM aipigania zabibu

Kilimo cha zabibu

Spread the love

JOEL Mwaka, Mbunge wa Jimbo la Chilonwa (CCM), amehoji serikali kwamba ina mpango gani wa kuhakikisha wataalam wa kilimo cha zabibu, wanapatikana ili kuwasaidia wakulima? Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Pia ametaka kujua mpango wa serikali wa kuanzisha bodi ya zabibu ili kukuza kilimo hicho.

Wizara ya Kilimo ikijibu swali hilo imeeleza, wizara hiyo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) – Makutupora, ina jukumu la kuzalisha na kusambaza teknolojia bora za kilimo cha zabibu.

Na kwamba, pia ina wajibu wa kuhakikisha wataalam wa kilimo cha zabibu katika Mkoa wa Dodoma na maeneo mengine nchini, wanajengewa uwezo ili kuwasaidia wakulima wa zabibu.

Imeeleza, mwaka 2019 wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine kama Kilimo Endelevu Tanzania (Sustainable Agricultural Tanzania) na Faida Mali, imefanikiwa kusambaza teknolojia bora za zabibu kwa wakulima na wadau mbalimbali 3065 katika kata za Chihanga na Makutupora.

“Ili kuongeza utaalam kwa watafiti wa TARI-Makutupora kuhusiana na taaluma ya mizabibu, taasisi hiyo imeendelea kuwawezesha watalaam wake kupata mafunzo ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kwenye nchi zilizobobea katika kilimo cha mizabibu kama vile Afrika Kusini na Ujerumani.

“Aidha, utaalam na uzoefu utakaopatikana utafikishwa kwa wagani na wakulima wa mfano ili kuzalisha zao hilo kwa tija na kulingana na vigezo vya masoko,” imeeleza wizara.

Imeeleza, kwa sasa wizara haina mpango wa kuanzisha Bodi ya Zabibu, badala yake wizara ipo kwenye hatua za awali za mapendekezo ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mazao ya Bustani.

error: Content is protected !!