January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge Bashungwa aanza kazi Karagwe

Spread the love

INNOCENT Lugha Bashungwa (37), aliyeshinda ubunge katika Jimbo la Uchaguzi la Karagwe, Mkoani Kagera, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), hatimaye amekula kiapo cha ubunge mjini Dodoma, mnamo 17 Novemb 2015. Katika uchaguzi huo, Bashungwa alipata kura 57,322 sawa na asilimia 55. Anaandika Deusdedit Kahangwa … (endelea).

Kuhusu elimu, Bashungwa anayo elimu ya juu inayohusisha uzoefu wa kimataifa, akiwa amebobea katika masuala ya uchumi na fedha.

Bashungwa alisoma darasa la kwanza mpaka la nne katika Shule ya Msingi ya Ahakishaka iliyoko Wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera, hapa Tanzania.

Kisha, kati ya mwaka 1991 mpaka 1993 alisoma darasa la tano mpaka la saba akiwa katika Shule ya Msingi ya Ubungo Kisiwani iliyoko mkoani Dar es Salaam, hapa Tanzania.

Kati ya mwaka 1994 na 1997 Bashungwa alisoma kidato cha kwanza mpaka cha nne katika shule ya sekondari ya Azania iliyoko Dar es Salaam, hapa Tanzania.

Kisha, Bashingwa alifanya masomo ya kidato cha tano na sita tangu mwaka 1998 mpaka 2000 katika taasisi iitwayo “Lake Region State College,” huko Marekani.

Na baadaye, Bashungwa alifanya shahada ya kwanza tangu mwaka 1998 mpaka 2000, akiwa anasomea uchumi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu John, huko Marekani.

Kisha, Bashungwa alifanya shahada ya pili tangu mwaka 2000 mpaka 2002, akiwa anasomea uchumi na fedha, katika Chuo Kikuu cha Colombia, huko Marekani.

Kuhusu uzoefu wa kazi, Bashungwa anao uzoefu wa utawala na uongozi wa kutosha ndani nan je ya Tanzania.

Tangu mwaka 2002 mpaka 2008, Bashungwa amefanya kazi katika taasisi iitwayo “World Institute for Leadership and Management in Africa (WILMA).” Taasisi hii inayo makao yake makuu huko Washington, Marekani. Pia inalo tawi lake Dar es Salaam, hapa Tanzania. Alifanya kazi kama “Program Manager for Tanzania.”

Mwaka 2009, Bashungwa alifanya kazi makao makuu ya Benki ya Dunia, Washington, Marekani katika kitengo kinachoshugulikia Afrika katika masuala ya “Finance and Private Sector Development.”

Pia, mwaka 2009, Bashungwa alifanya kazi katika taasisi iitwayo “Research for Development (R4D)” ya Washington, Marekani. Kati ya mwaka 2010 na 2011 alifanya kazi katika taasisi iitwayo “Leader Creek Fisheries” iliyoko Naknek, huko Marekani.

Na tangu mwaka 2012 mpaka anachaguliwa kuwa Mbunge wa Karagwe amefanya kazi kama mchumi katika Wizara ya Nishati na Madini ya Tanzania.

Bashingwa amekuwa mbunge wa Wilaya iliyoko Magharibi mwa Ziwa Viktoria, ikiwa inapakana na Wilaya ya Kyerwa kwa upande wa Kaskazini; nchi ya Rwanda kwa upande wa Kusini Magharibi; Wilaya ya Ngara kwa upande wa Kusini; na Wilaya ya Missenyi, Bukoba na Muleba kwa upande wa Mashariki.

Katika wilaya hii, Bashungwa ni mbunge wa saba tangu wilaya hii ilipopata mbunge wa kwanza mwaka 1965. Kabla ya mwaka 1965, Karagwe ilikuwa sehemu ya “Mkoa wa Ziwa Magharibi” uliojumuisha wilaya nne za Ngara, Biharamuro, Karagwe na Bukoba. Wilaya hizi zilikuwa zinatawaliwa kwa njia ya mkono wa mbali kuanzia makao makuu ya mkoa huo yaliyokuwa Mwanza.

Kihistoria, wabunge waliomtangulia Bashingwa ni Gervase Kaneno(1965–1968), Laurent Nyamalaba(1968–1975), Venant Rwabuti(1975–1980), Elikano Byeitima (1980–1995), George Kahama(1995–2005), na Gosbert Blandes (2005–2015).

Kiutawala, Bashungwa atafanya kazi pamoja na Maafisa Tarafa 5, Watendaji wa Kata 23, Watendaji wa Vijiji 77, Watendaji wa Vitongoji 629, wakiwahudumia watu wapatao watu 351,556 waliotawanyika katika eneo la kilomita za mraba 4,500. Takwimu hizi zimekokotolewa kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, inayoonyesha kwamba Karagwe ilikuwa na watu 332,020, wanaoongezeka kwa kasi ya asilimia 2.9 kila mwaka.

Bashungwa amekuwa mbunge wa Wilaya ya watu maskini. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi 2012, kipato cha wastani cha mwananchi kwa mwaka kilikuwa Sh.475,000/=. Katika mwaka 2015 inakadiriwa kwamba mwananchi wa Karagwe anapata Sh. 520,000 kwa mwaka.

Wananchi wa Karagwe wanapata fedha hizi kutokana na kilimo cha mazao kama vile kahawa, ndizi, na maharage; na ufugaji wa ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku. Mchango wa sekta hizi katika kipata cha mwananchi wa Karagwe ni kama ifuatavyo, mchango ukiwa kwenye mabano: kilimo(80%), shughuli za biashara (5%), watumishi wa kazi za ofisini (3%), ufugaji (10%), na shughuli nyingine 3%.

Kwa ujumla, udogo wa kipato cha wananchi wa Karagwe, kilicho chini ya dola moja kwa siku, unamweleza vizuri Bashungwa ugumu wa maisha unaowakabili wananchi wake.

Ni wazi kwamba, kati ya wananchi kumi wanaogusa mifukoni ili kulipa karo za watoto, kulipia huduma za matibabu, kununua mavazi, kununua vifaa vya ujenzi wa nyumba bora, au kununua malazi, ni watatu pekee wanaoweza kutimiza haja za mioyo yao. Huu ndio msalaba alioubeba Bashungwa.

Akiongea na mwandishi mara baada ya kuapishwa mjini Dodoma, Bashungwa aliwashukuru wapiga kura wa Karagwe kwa kuonyesha imani kwake.

“Nina deni kubwa kwa wapiga kura wangu. Nimeizunguka Karagwe na kufahamu matatizo yake katika sekta zote za maisha ya wananchi. Kwa kunichagua wanataka nisimame katikati yao na matatizo haya. Nami nitatumia social connections (mahusiano ya kijamii) nilizo nazo ndani na nje ya Karagwe kupigania ujio wa Karagwe mpya,” alisema Bashungwa.

Bashubgwa aliendelea : ‘Wakati wa kampeni wananchi walionyesha shauku ya kuwa na mbunge anayewapa mrejesho. Hilo nitalizingatia. Nitakuwa nawapa taarifa hatua kwa hatua kuhusu mipango ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Karagwe. Mafanikio na matatizo ninayokumbana nayo watayafahamu kwa wakati ili tuweze kusonge mbele pamoja.”

Bashungwa anaamini kwamba Kamati za Kudumu za Baraza la Madiwani zitamsadia kufanikisha mipango aliyo nayo. “Hivi sasa nakimbia kwenda Karagwe ili kushiriki katika kuunda kamati mbalimbali za Baraza la Madiwani ili tuweza kuanza kazi mara moja. Kamati hizi zinayo nafasi kubwa ktika ujenzi wa Karagwe mpya,” alisema Bashungwa.

Mwisho anawaomba wananchi wa Karagwe kufanya kazi kwa umoja bila kujali tofauti zao za kikabila, kidini, au kiitikadi ili kufanikisha ujenzi wa Karagwe mpya. “Naamini kwamba umoja ni ushindi. Hivyo nawaomba wananchi wote wa Karagwe wanipe ushirikiano ili niweze kuwatumikia kwa kutimia kila kipaji nilichopewa na Mwenyezi Mungu,” anamalizia Bashungwa.

Bashungwa alimwoa Jennifer John(34). Mpaka sasa wamebarikiwa watoto watatu, ambao ni Santo Baraka(8) ambaye ni mvulana, Solana Coletha(3) ambaye ni msichana, na Sankara Stan(3) ambaye ni mvulana. Solana na Sankara ni mapacha.

error: Content is protected !!