June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge awataka wananchi kutokwamisha miradi

Spread the love

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa (CCM), amewataka wananchi kuacha ukwamisha utayarishaji wa miradi mbalimbali katika jimbo hilo, ikiwa ni pamoja na kutaka malipo makubwa ya fidia ili kuruhusu miundombinu kupita katika maeneo yao. Anaandika Hamisi Mguta, Kibaha … (endelea).

Hamoud amezungumza hayo katika mahojiano na MwanaHALISI Online kuhusu miradi mbalimbali inayoendelea kufanyika katika jimbo lake ambayo mara kadhaa imekuwa ikilalamikiwa na wakazi wa jimbo hilo kuwa haiwanufaishi kutokana na ujira mdogo unaotolewa na waajiri katika miradi.

Amesema kuwa suala la miradi inayoanzishwa katika jimbo hilo limekuwa likikwamishwa na wananchi wenyewe kwa kudai fidia kubwa ili kupisha miundombinu kama, mabomba na nguzo za umeme.

Hamoud amesema miongoni mwa miradi iliyoonekana kukwamishwa ni mradi wa umeme vijijini, kutokea Mlandizi hadi Mzenga ambapo baadhi ya wananchi walihitaji fidia kubwa kuruhusu upitishwaji wa nguzo za umeme katika maeneo yao bila kujali mradi utawanufaisha wakazi wote jimbo la Kibaha Vijijini.

“Ukiachana na mradi wa umeme, hata mwekezaji wa kiwanda cha chuma cha Disunyara, baadhi ya watu wanataka walipwe fidia kubwa sasa hapo tutaliendelezaje jimbo kama wananchi wenyewe wanakwamisha?” amesema Hamoud.

Kuhusu suala la ujira mdogo, Hamoud amesema kuwa hana uwezo wa kufanya malipo yaongezeke kwa wafanyakazi kutokana na suala la ajira kuwa la kisheria, makubaliano baina ya mwajiri na mwajiriwa.

Hamoud amesema: “Kipo kiwanda kimoja cha chuma huko Disunyara, ndio kinaelekea kukamilika, nitahakikisha upatikanaji wa ajira kwa wakazi wa jimbo langu ili wanufaike na mradi huo na mingine inayoendelea kuja laikini sio kuwapangia waajiri kiasi cha kuwalipa wafanyakazi.”

“Unajua hakuna asiyehitaji kuongezewa mshahara lakini kwa Mbunge hawezi kumuamuru mwajiri aongeze mshahara, kikubwa tutahakikisha tunapata wawekezaji wa viwanda kwa wingi ili watu wapate ajira na wananchi waunge mkono waachane na kuweka vikwazo vya maendeleo.”

error: Content is protected !!