RUKIA Kassim Ahmed, Mbunge Viti Maalumu kupitia Chama cha Wananchi (CUF), ameitaka Serikali ya Tanzania kuwazuia wanaume wasiotahiriwa kuoa, ili kuwakinga wanawake dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Rukia ametoa hoja hiyo leo Jumanne tarehe 9 Juni 2020, wakati akiuliza swali kuhusu mkakati wa serikali katika kuweka zuio la kuoa kwa wanaume ambao hawajatahiriwa.
“Imethibitika kuwa saratani ya mlango wa kizazi inasababishwa na virusi vinavyopatikana kwa wanaume ambao hawajatahiriwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka zuio la kuoa kwa wanaume ambao hawajatahiriwa,” ameuliza swali hilo kwa njia ya mtandao wa Bunge.
Akijibu swali hilo kwa njia hiyohiyo, Waziri wa Afya amesema, Serikali haina mkakati wa kuweka zuio hilo, bali imeweka mikakati dhidi ya kujikinga na Kirusi cha Human Papiloma, kinachosababishwa saratani hiyo, kwa njia ya kujamiiana.
“Serikali imeweka mikakati dhidi ya kujikinga na kirusi hiki ikiwemo utoaji wa chanjo dhidi ya kirusi cha papilloma kwa wasichana wa umri ya miaka 9-14 kote nchini, “ amesema Waziri wa Afya.
Sambamba na chanjo hiyo, Waziri wa Afya amesema, Serikali inaendelea kuhamasisha wanaume kufanya tohara, kwa kuwa wanaume hao wako kwenye hatari ya kuwa na kirusi hicho, kinachosababisha saratani.
“Tunahakikisha tunatoa elimu juu ya kubadilisha tabia, ikiwepo pia kuhamasisha kufanya tohara kwa wanaume, kwani wanaume waliofanyiwa tohara hawapo kwenye hatari ya kuwa na kirusi hiki (cha Papiloma) kinachosababisha saratani,” amesema Waziri wa Afya.
Waziri huyo amesema, “kwa wale wanawake ambao wameshapata maambukizo ya kirusi cha papilloma, tunahamasisha kufanya uchunguzi wa kutambua uwepo wa mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi na kuwapatia tiba ya ugandishaji kwa kutumia kimiminika cha gesi ya carbondioxide.”
Leave a comment