MBUNGE wa Vunjo mkoani Kilimanjaro (CCM), Dk. Charles Kimei, ameiomba Serikali irudishe fedha za kodi zilizokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwenye taasisi za dini, kinyume cha sheria. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).
Akizungumza bungeni jijini Dodoma, leo Jumanne tarehe 25 Mei 2021, Dk. Kimei amedai kuwa, utendaji wa taasisi hizo umezorota, baada ya kushinikizwa na baadhi ya maafisa wa TRA, walipe kodi.
Wakati huo huo, Dk. Kimei, aliiomba Serikali iwachukulie hatua maafisa hao, wanaodaiwa kuzishinikiza taasisi za dini, kulipa kodi kinyume cha sheria.
“Serikali itakuwa tayari kurejesha kodi zilizokusanywa katika taasisi hizo kwa shinikizo na hatimaye kuzidhoofidha sana? Pili, Serikali iko tayari kuchukua hatua za kinidhamu kwa maafisa wa TRA wanaokiuka sheria?” amesema Dk. Kimei.
Mbali na maombi hayo, Dk. Kimei aliiomba Serikali isamehe madeni ya kodi za muda mrefu, ya taasisi za dini, zilizokuwa zinajiendesha kwa utaratibu wa kutopata faida.
“Je, Serikali haioni umuhimu wa kuzisamehe kodi za miaka ya nyuma taasisi za dini, zilizokuwa zikiendeshwa kwa utaratibu usiolenga kupata faida. Na kuziwekea utaratibu wa kuanza kulipa tangu walipojulishwa utaratibu wa kuanza kulipa kodi?” amesema Dk. Kimei.
Akijibu maombi hayo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itafanyia kazi maombi hayo, na ikibainika taasisi hizo zilitozwa kodi kinyume cha sheria, itazirejesha fedha hizo.

“Serikali ina utaratibu wa kurejesha fedha ambazo zilichukuliwa na kwa mujibu wa sheria, inatakiwa kurejeshwa kwa utaratibu wa kawaida wa kufanya refunding,” amesema Dk. Nchemba.
Kuhusu maafisa TRA wanaodaiwa kukiuka sheria, Dk. Nchemba amesema Serikali itafanya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo na kwamba ikibainika wana makosa, itawachukuliwa hatua za kinidhamu.
“Na meneo ambayo kuna amkosa ya ukiukwaji sheria, taratibu za kisheria hufuatwa na hatua stahiki za kinidhamu huchukuliwa kwa wanaokiuka sheria. Kama kuna meneo maafisa wetu wamekiuka sheria, taratibu za kisheria zitachukuliwa,” amesema Dk. Nchemba.
Akizungumzia ombi la taasisi hizo kusamehewa madeni, Dk. Nchemba amesema Serikali inaendelea kufanya tathimini juu ya maombi hayo, kwa ajili ya kuchukua hatua.
“Serikali imekuwa ikipokea maombi ya kusamehe kodi za miaka ya nyuma toka taasisi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na taasisi za Dini. Serikali inaendelea kutathmini maombi hayo, ili kuona hatua zinazoweza kuchukuliwa bila kuathiri matakwa ya sheria zilizopo,” amesema Dk. Mwigulu.
Leave a comment