MBUNGE wa Wingwi, Omary Issa Kombo (CCM), ameitaka Serikali iongeze fedha za mfuko wa jimbo katika majimbo yenye uhitaji mkubwa, ikiwemo jimbo lake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Kombo ametoa ombi hilo bungeni jijini Dodoma, leo tarehe 6 Novemba 2023, alipoihoji Serikali inatumia vigezo gani kugawa fedha hizo na lini itafanya tathimini kwa kuzingatia vigezo na ugawaji wake, ili majimbo yenye idadi kubwa ya watu yaongezewe fedha.
“Ni lini Serikali ilifanya tathimini kwa kuzingatia vigezo hivi sambamba na mgawnayo wa fedha za majimbo? Tunashuhudia baadhi ya majimbo yakipata fedha kidogo ikizingatia vigezo alivyoeleza waziri, serikali haina haja kufanya tathimini ya vigezo hivi kwa kuzingatia matokeo ya sensa ya watu na makazi ya 2022,” amesema Kombo
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dk. Festo Dugange, amesema vigezo vinavyotumika katika ugawaji wa fedha za jimbo ni idadi ya watu kwa asilimia 45, mgawo wa kila jimbo (25%), kiwango cha umaskini (20%) na ukubwa wa eneo (10%).
Dk. Dugange amesema serikali inaendelea kufanya tathimini mara kwa mara ili kubaini namna nzuri ya kuboresha viwango vya ugawaji fedha za majimbo.
“Serikali inafanya tathimini mara kjwa mara kuhakikisha kwamba vinakidhi mahitaji ya fedha za mfuko wa jiumbo katika majimbo yetu, kuona namna nzuri ya kuendelea kuboresha fomula za vigezo viweze kutoka fedha. Serikali itaendelea kufanya tathimini ikionekana kuna maeneo vigezo vinatakiwa kuongezwa vitafanyika,” amesema Dk. Dugange.
Leave a comment