July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge apinga watumishi waliotenguliwa kushushwa mishahara

Ukumbi wa Bunge

Spread the love

 

MBUNGE wa jimbo la Kilwa Kusini nchini Tanzania, Ally Kassinge, amepinga hatua ya Serikali kutaka kushusha mishahara ya watumishi wanaomaliza nafasi zao za uteuzi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Kassinge amesema kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma watu hao wanapashwa kuendelea na mshahara wao hata baada ya uteuzi wao kukoma.

Akitetea hoja hiyo Kassinga amesema mtumishi anapopata nafasi ya uteuzi barua ya uteuzi huwa inaeleza kuwa mtumishi huyo pia amepandishwa cheo.

“Mtumishi anapoteuliwa kwenye nafasi ya uteuzi aidha alikuwa afisa daraja la kwanza, afisa mwandamizi, afisa wa juu au ofisa mkuu anapopata barua ya uteuzi inamweleza kwamba umepandishwa cheo na kupata uteuzi,” amesema Kassinga.

Amesema utumishi wa umma unazingatia Sera ya Menejimenti na Ajira ya mwaka 1999, Sheria ya Utumishi Umma ya mwaka 2002, Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2013, Kanuni za Kudumu za Utumishi za mwaka 2019, Kanuni za Uongozi Bora, Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini na miongozo mbalimbali inayoongoza utumishi wa umma, “kama hivyo ndivyo Serikali tunakwama wapi? Sheria hizo kanuni, miongozo hii tuliitunga wenyewe kwanini hatuzingatii utaratibu?” amehoji.

“Sasa unapomteua na kumpandisha cheo unamtoa kwenye daraja lile na maslahi anayopata ikiwemo mshahara wake ni kwasababu umempandisha cheo, sasa uteuzi wake unapokoma ndiyo inamfanya abaki na mshahara ule alioteuliwa nao kwasababu alipandishwa cheo,” amesema.

Ameongeza “kwa maana hiyo napendekeza kuwa watumishi hawa wanapomaliza nafasi za uteuzi wasipunguziwe mshahara wao.”

Amesema kupandishwa cheo “si adhabu, kupandishwa cheo ni tija, ni faraja na ni heshima sasa inakuwaje unamvunjia ile heshima, nishauri serikali mpango wake wa kuwashusha mshahara waliotenguliwa isiendelee nao.”

Pia Mbunge huyo amesema kumekuwepo na hali ya kutosimamia vyema eneo la utumishi wa umma hususan eneo la pensheni na stahiki za watumishi.

“Eneo la Pensheni watumishi wanacheleweshewa, wapo watu wamestaafu mika miwili, mitatu iliyopita lakini hadi sasa hawajapata mafao yao na malipo ya kuwasafirisha mizigo.”

Ameitaka Serikali kuwa zoezi la kusafisha taarifa za watumishi liende sambamba na Serikali kujisafisha yenyewe kwa kulipa madeni.

error: Content is protected !!