January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge Anatropia wa Segerea afunguka

Spread the love

MBUNGE wa Viti Maluum (Chadema), kupitia mkoa wa kichama wa Ilala, Anatropia Theonest, amefunguka na kuliambia gazeti la mwanahalisionline kwamba yeye ni ‘jembe’ la uhakika ndani na nje ya Chadema, na kwamba anamshukuru Mungu kwa kumruhusu ndoto yake kutimia mwaka huu. Anaandika Deusdedit Kahangwa …. (endelea).

Akiongea na mwandishi wa habari hii nyumbani kwake Segerea, jijini Dar es Salaam, Anatropia alisema: “Pamoja na utata wote ulioripotiwa na vyombo vya habari kuhusu uteuzi wangu, naamini kwamba mimi ni mbunge halali wa Chadema, lakini mwenye dhamana ya kuwatumikia Watanzania wote kwa kutumia elimu, uzoefu, ubunifu, uwezo na ujasiri niliojaliwa na Mungu. Nakishukuru Chama changu cha Chadema kwa kutambua utayari wangu wa kuwatumikia wananchi.”

Awakosoa wapinzani wa uteuzi wake

Uteuzi wa Anatropia kama mbunge wa viti maalum kupitia jimbo la Chadema la Segerea ulizua sintofahamu iliyoripotiwa katika vyombo vya habari katika sura ambayo ilionekana kutishia umoja wa UKAWA huko jimboni Segerea.

Lakini, kwa maoni ya Aanatropia, mgogoro huo umekuzwa sana pasipo sababu za msingi. Kuhusu mgogoro huu, anajieleza kwa kirefu akisema:

“Mimi niligombea ubunge ndani ya Chadema na kushinda kura za maoni. Nikaanza mchakato wa kiserikali mpaka nikazindua kampeni.

“Baada ya hapo ndipo nilipata taarifa kwamba mgombea wa UKAWA ni Julius Mtatiro wa CUF.

“Nilikwenda mahakamani kula kiapo ili kujitoa ulingoni kwa lengo la kuimarisha umoja wetu ndani ya UKAWA.

“Kwa bahati mbaya, 25 Oktoba 2015 siku ya uchaguzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilileta karatasi za kura zenye jina na picha yangu.

“Hivyo, wananchi wakanipigia kura kwa sababu hiyo. Nilipata kura 48,623 wakati Mtatito alipata kura 75,744.

“Lakini, kusema kweli, nilipokuwa jukwaani wakati wa kampeni nilimnadi Julius Mtatiro wa CUF.”

Kwa ajili ya kuthibitisha madai yake haya, Anatropia alimpatia mwandishi wa habari hizi kipande cha video kinachomwonyesha Anatropia wa Chadema akimwombea kura Mtatiro wa CUF.

Anatropia pia alitoa nakala ya gazeti la Mwananchi la 25 Oktoba 2015, likimnukuu Mtairo akithibitisha kwamba, ni kweli kuwa “Anatropia… kama mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea kwa tiketi ya Chadema … alishajitoa.”

Julius Mtatiro, ambaye alikuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CUF, chini ya mwavuli wa UKAWA jimbo la Segerea alikuwa anailalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kulibakiza kimakosa jina la Anatropia Theonest wa Chadema kwenye karatasi ya mpiga kura wakati walishakubaliana amejitoa.

Mtatiro aliliambia gazeti la Mwananchi kwamba, kadhia “hiyo inaweza kuwachanganya wapiga kura,” na kesho yake gazeti hili likaandika habari kuu ikiwa na kicha cha maneno, “NEC waacha jina la mgombea aliyejitoa Jimbo la Segerea.”

Kwa sababu hizi, Anatropia anahitimisha sintofahamu hii kwa kusema:

“Kwa hiyo, ninasikitika kusikia lawama zinazoelekezwa kwangu zikidai kwamba mimi ndiye nimesababisha jimbo la Segerea liende CCM. Nawaomba wana Chadema na wana UKAWA kuutambua ukweli hii ili tusonge mbele kama kitu kimoja. Kuna maisha baada ya uchaguzi.”

Akanusha kuvuliwa uanachama

Alipoulizwa kuhusu habari zilizozagaa kwenye vyombo vya habari kwamba yeye Anatropia amevuliwa uanachma na uongozi wa Chadema Jimbo la Segerea, alijibu kwa haraka kwamba yeye bado ni mwanachama halali wa Chadema.

Alipotakiwa kufafanua usemi wake alijibu kwamba, “Chadema ni taasisi inayoendeshwa kwa mujibu wa Katiba, kanuni na taratibu.”

Kwa haraka alinyanyua nakala ya Kanuni za Chadema (2006), na kuisoma ibara ya 6.52 kwa sauti. Ibara hiyo inasema yafuatayo:

“… mwanachama yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu ama kuonywa ama kuachishwa ama kufukuzwa uanachama bila kwanza: (a) kujulishwa makosa yake kwa maandishi na kutakiwa kutoa majibu katika muda usiopungua wiki mbili. (b) Kupewa nafasi ya kujitetea mbele ya kikao kinachohusika. (c) Mwanachama atajulishwa kwa maandishi uamuzi wa kikao mnamo wiki mbili baada ya kusikilizwa.”

Anatropia anasema hajawahi kuhojiwa na kikao chochote kuhusu tuhuma zozote; na kwamba, hajawahi kupewa barua yoyote akitaarifiwa kuhusu kukoma kwa uanachama wake.

“Hivyo, ninazichukulia taarifa kwamba nimepokonywa uanachama wangu wa Chadema kama maneno ya mitaani,” alihitimisha Anatropia.

Elimu na taaluma

Alipoulizwa kuhusu elimu yake, Anatropia alisema: “mimi ni msomi mwenye shahada ya pili kutoka kutoka Chuo Kikuuu cha Mzumbe katika masuala ya biashara na utawala (MBA). Nilitunikiwa shahada hiyo mwaka 2012.”

Anatropia alimwambia mwandishi wa habari hii kwamba yeye pia ni mwalimu aliyepata shahada ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2008.

“Ndugu mwandishi, kwa elimu na uzoefu wangu naamini kwamba niko katika nafasi nzuri ya kuwatumikia Watanzania. Chadema hawajakosea kuniibua kupitia mchakato wa viti maalum. Sema tu watu wengi hawanifahamu ndiyo maana wananibeza. Lakini nitahakikisha wananifahamu vizuri kupitia matendo yangu,” alisema Anatropia.

Haiba na tabia yake

Anatropia Theonest ni mama mchangamfu, mwenye kujiamini na mwenye haiba iliyo kati ya watu wakimya sana (introverts) na watu waongeaji sana (extroverts).

Kuhusu mtazamo wake kuhusu kazi na mahusiano yake na watu anasema, “mimi ni mama mjasiriamali ambaye nimekuwa natumia sehemu ya kipato changu kuwaunganisha wananchi wa Segerea katika taabu na raha. Ninao wafuasi wengi kwa sababu sibagui mtu.”

Anachosema hapa Aanatropia ni kwamba, kwa upande mwingine, haiba yake, inamweka katikati ya watu wanaojali kazi tu kuliko watu (work-oriented persons) na watu wanaojali majirani zao zaidi kuliko kazi (people-oriented persons).

Maisha yake ya familia

Kuhusu maisha ya familia, anatropia alimwambia mwandishi kwamba, ameolewa na anao watoto wawili, Lightness(6) na Lynette(2).

“Mme wangu ni Angelo Aloyse, Tumebahatika kupata watoto wawili, Lightness mwenye miaka sita na Lynette mwenye miaka miwili,” anasema Anatropia.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema amwongelea Anatropia

Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, akiongea na mwandishi wa habari hii, alieleza kwa kirefu jinsi wabunge wa viti maalum ndani ya Chadema walivyopatikana.

“Nafasi za ubunge wa viti maalum ndani ya Chadema zilitolewa kwa makundi maalum matatu. Makundi hayo ni kundi la uwakilishi wa mikoa, kundi maalum, na kundi la nafasi za aliyekuwa mgombea urais wetu.

“Katika kundi maalumwaliteuliwa wabunge wawili, kundi la mgombea urais wabunge wanne, na kundi la uwakilishi wa mikoa wabunge 30. Anatropia Theonest alipatikana kwa mujibu wa utaratibu huu wa kikanuni. Hivyo, ni mbunge mteule halali anayesubiri kuapishwa.

“Lakini kama kuna mtu anayo malalamiko ayalete na tutayashughulikia kwa mujibu wa taratibu za chama, na sio vinginevyo.”

Mbunge mteule Anatropia Theonest anakusudia kwenda Dodoma wikendi hii kwa ajili ya kula kiapo na kuanza kazi mara moja.

error: Content is protected !!