MBUNGE wa Kwela, Deus Sangu, amewasilisha hoja ya dharura bungeni jijini Dodoma, akitaka kikao cha Bunge kiahirishwe kwa muda ili kujadili mgogoro sugu wa ardhi kati ya wananchi na mwekezaji wa shamba la Malonje, Efatha Ministry, baada ya kuibuka mauaji ya raia yanayodaiwa kufanywa na walinzi wa taasisi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Akiwasilisha hoja hiyo bungeni jijini Dodoma, leo tarehe 7 Novemba 2023, Sangu amedai licha ya Waziri wa Ardhi, Jerry Silaa, kuahidi kutembelea katika shamba hilo ili kutatua mgogoro tarehe 17 Novemba mwaka huu, jana tarehe 6 Novemba mwaka huu, mauaji hayo yametokea.
Sangu amedai kuwa, ameamua kuwasilisha hoja hiyo baada ya kulalamika bungeni zaidi ya mara tatu, lakini Serikali imeshindwa kuchukua hatua madhubuti, kitendo alichodai kuwa kinapelekea wananchi wa eneo husika kuendelea kunyanyasika.

Mbunge huyo wa Kwela, mkoani Rukwa, amedai walinzi wa Efatha Ministry jana waliwashambulia kwa risasi wananchi na kuwasababishia majeruhi huku baadhi yao wakipoteza maisha.
“Waziri wa Ardhi aliahidi atafika tarehe 17 Novemba 2023, lakini kabla hajafika limetokea tukio la ajabu sana, askari wanaolinda shamba hilo wamewapiga wananchi waliokuwa shambani risasi na kuwanyang’anya ng’ombe 42. Waliojeruhiwa ni Danson Charles aliyepigwa risasi ya tumboni na Festo Kamwanga, aliyepigwa risasi moja kifuani,” amedai Sangu.
Sangu amedai “haya yote nimeyaeleza lakini sijui nini kinachotokea, au kwa makusudi au kwa maslahi yaliyojificha hili jambo halijashughulikiwa. Hawa walinzi wamekuwa wakiwabaka kina mama hadi sasa 10 wamebakwa, wananchi walikatwa masikio,”
“Huyu mwekezaji ni nani ambaye anachukua mamlaka makubwa kutaka kuuwa watu? Wananchi wangapi wafe ndio Serikali ichukue hatua?”
Baada ya Sangu kuwasilisha hoja hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Daniel Sillo, aliitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, itoe ufafanuzi.
Naibu Waziri wa Ardhi, Geofrey Pinda, alikiri mauaji hayo kutokea huku akiahidi watafika eneo la tukio kwa ajili ya kumaliza mgogoro huo.
Kufuatia majibu hayo, Sillo aliitaka wizara hiyo ikifike haraka katika eneo la mgogoro huo kwa ajili ya kuchukua hatua.
“Niombe Serikali iende eneo la tukio haraka iwezekanavyo kwenda kuangalia hali ya majeruhi namna gani ya kuwasaidia kwa matibabu na kushiriki mazishi ya wengine waliopoteza maisha,” amesema Sillo.
Leave a comment