MBUNGE wa Viti Maalum (Chadema), Zubeda Sakuru, ametaka kujua kwa nini wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya ufundi stadi (Veta) kukosa mikopo. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea)
Zubeda ameuliza swali bungeni leo Alhamisi tarehe 28 Mei, 2020 kwa njia ya mtandao na kujibiwa na mfumo huo huo na waziri wa elimu, sayansi na teknolojia.
“Kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya ufundi stadi (Veta), lakini wanafunzi waliojiunga na vyuo hivyo hawapati mikopo kutoka serikalini. Je, Serikali itaanza lini kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya ufundi stadi,” ameuliza Zubeda.
Akijibu swali hilo, waziri wa elimu, sayansi na teknolojia amesema, kwa sasa mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (SURA 178) ambayo inawabainisha walengwa ni Watanzania wahitaji walioomba mkopo na wenye sifa za kujiunga na taasisi za elimu ya juu na sio vyuo vya ufundi stadi.
“Serikali imeendelea kutambua kuwepo kwa umuhimu mkubwa wa mafunzo ya ufundi stadi kama kipaumbele chetu cha kujenga uchumi wa viwanda.”
“Hivyo, Serikali imeendelea kubeba gharama nyingi za vyuo vya ufundi stadi vya Serikali ambavyo havilengwi na sheria hiyo ili ada zao ziwe nafuu na Watanzania wa kawaida waweze kumudu,” amesema
Amesema, Serikali inaendelea kupanua upatikanaji wa fursa hizo za masomo hayo ya ufundi stadi kwa kujenga vyuo vipya hasa maeneo ya vijijini ambayo yalikuwa hayana vyuo hivi.
“Kwa sasa, utaratibu utaendelea kuwa huo huo wa Serikali kuvipa vyuo hivyo vya ufundi stadi ruzuku ili kumpunguzia mwananchi wa kawaida gharama za kusoma.”
“Hata hivyo, maoni ya Zubeda Sukuru na wadau wengine yanaendelea kupokelewa ili kuboresha utaratibu wa sasa kwa kadri uchumi wetu unavyoendelea kuimarika,” amesema
Leave a comment