AYSHAROSE Mattenbe, Mbunge viti maalumu (CCM), ameitaka serikali kuona umuhimu wa kuzijenga barabara zinazounganisha jimbo la Singida Kaskazini mkoani humo. Anaripoti Jemima Samwel, DMC … (endelea).
Ameyasema hayo leo Jumanne, tarehe 18 Mei 2021, katika kipindi cha maswali na majibu, bungeni jijini Dodoma.
Mbunge huyo amesema, serikali inapaswa kutambua umuhimu wa barabara hiyo kwa sababau ndiyo inayoonganisha vijiji vyote vya Singida Kaskazini.
“Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza barabara za Singida Kaskazini, zinazounganisha Vijiji ambazo hazipitiki kwa sasa?”
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Tamisemi, David Silinde amesema, Singida Kaskazini ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 811.68 ambao umekuwa ukifanyiwa matengenezo pamoja, kujenga na kukarabati vivuko.
“Katika mwaka wa fedha 2019/20, Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (Tarura), Halmashauri ya Wilaya ya Singida, ilifanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 78.55 na vivuko 22 kwa gharama ya Sh.739.39 milioni.”
“Katika mwaka fedha 2020/21, barabara zenye urefu wa kilomita 67.8 na vivuko 20 vimetengenezwa kwa gharama ya Sh. 711.08 Milioni ambapo hadi Machi 2021 barabara zenye urefu wa kilomita 45 na vivuko 15 vimekamilika,” ameeleza Silinde.
Pia, katika mwaka wa fedha 2021/22 barabara zenye urefu wa kilomita 62.5 na vivuko 24 vitajengwa kwa gharama ya Sh. 711.08 Milioni
“Serikali kupitia Tarura, halmashauri ya wilaya ya Singida, itafanya tathmini ya barabara zote za Singida Kaskazini ili kuandaa mpango wa namna bora ya kuweka vipaumbele vya ujenzi na matengenezo ya barabara,” amesema Silinde.
Leave a comment