May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbunge ahoji mashamba kutaifishwa, Lukuvi amjibu

Cesilia Pareso, Mbunge wa viti maalumu

Spread the love

 

MBUNGE Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Cecilia Pareso, amehoji Serikali itataifisha lini mashamba ya wawekezaji yasiyoendelezwa, ili yakabidhiwe kwa wananchi kwa ajili ya kutatua changamoto ya ukosefu wa ardhi Kata za Daa na Oldeani, mkoani Arusha. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma…(endelea).

Pareso aliyefukuzwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amehoji hayo leo Jumatano tarehe 3 Februari 2021, bungeni jijini Dodoma.

“Je, Serikali ina mpango gani wa kuyagawa kwa wananchi mashamba makubwa yanayomilikiwa na wawekezaji katika kata hizo, ambayo hayaendelezwi huku wananchi wakikosa ardhi ya makazi?” amehoji Pareso.

Akijibu swali la mbunge huyo, Waziri Wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema, Serikali ilifanya uhakiki na kugundua mashamba 25 ya wawekezaji katika kata hizo, ambapo tisa kati yake yameendelezwa.

“Taarifa za awali za uhakiki zinaonesha kuwa mashamba hayo yameendelezwa kwa viwango tofauti ,ambapo mashamba 9 yameendelezwa kwa wastani wa asilimia 50.

“Sehemu nyingine ya mashamba hayo imejengwa miundombinu ya barabara na huduma za kijamii kama vile shule, nyumba za kulala wageni, viwanda, vituo vya watalii,” amesema Lukuvi.

Lukuvi amesema, Serikali inaendelea kufanya uhakiki wa kina kwa mashamba yote, kwa ajili ya kuchukua hatua kwa wamiliki ambao wameshindwa kutimiza masharti ya umiliki.

“Kwa sasa, Serikali inaendelea kufanya uhakiki wa kina wa mashamba yote na kuchukua hatua kwa wamiliki ambao wameshindwa kutimiza masharti ya umiliki,” amesema Lukuvi.

Lukuvi amesema ‘Hatua zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kubatilisha milki za mashamba ambayo wamiliki wamekiuka masharti ya uendelezaji.”

Aidha, Lukuvi amesema katika kipindi cha miaka mitano (2015-2020)Serikali ilitaifisha mashamba 45 yenye jumla ekari 121,032.243 katika maeneo mbalimbali nchini, ya wawekezaji walioshindwa kuyaendeleza.

error: Content is protected !!