MBUNGE Viti Maalumu asiye na chama bungeni, Agnesta Lambart, amehoji lini Serikali itapeleka majisafi na salama katika Wilaya ya Butiama mkoani Mara, ili kuuenzi mchango wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Lambart alifukuzwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), tarehe 27 Novemba 2020, kwa tuhuma za usaliti, baada ya kuapishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwa mbunge viti maalumu, kinyume na taratibu za chama.
Lambart amehoji swali hilo leo Jumanne tarehe 30 Machi 2021, katika kipindi cha maswali na majibu, bungeni jijini Dodoma.
“Je, ni lini Serikali itapeleka majisafi na salama Butiama ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere katika Taifa letu,?” amehoji Lambart.

Mwalimu Nyerere alizaliwa Wilayani Butiama tarehe 12 Aprili 1922 hadi sasa Mjane wake, Mama Maria Nyerere anaendelea kuishi wilayani humo, tangu mwanasiasa huyo alipofariki dunia tarehe 14 Oktoba 1999.
Mwalimu Nyerere, alizikwa Butiama.
Akijibu swali la Lambart, Naibu Waziri wa Maji, Marryprisca Mahundi amesema, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa maji wa Mugango-Kiabakari- Butiama tangu Desemba 2020 ambao unatarajiwa kukamilika Desemba 2022.
“Kazi zilizoanza kutekelezwa katika mradi huo ni upimaji maeneo ya ujenzi wa matanki, mtambo wa kusafisha maji, njia kuu ya bomba na uletaji wa vifaa kwenye eneo la mradi.”
“Mradi huu unatarajiwa kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji kwa asilimia 100 katika eneo la mradi pamoja na vijiji vilivyopo ndani ya kilomita 12 kutoka bomba kuu,” amejibu Mahundi.
Amesema mradi huo unatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa Maendeleo wa Saudia (Saudi Fund for Development – SFD) kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 30.69 (Sh. 70 Bil.).
Aidha, Mahundi amesema, hali ya upatikanaji maji wilayani humo ni asilimia 61.18, na kwamba, Serikali inaendelea kukamilisha miradi ya maji ili kumaliza changamoto hiyo.
Naibu Waziri huyo wa Maji amesema, Serikali kupitia Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), imekamilisha miradi ya maji katika vijiji vya Nyabange, Magunga, Kongoto, Bukabwa, Kamgendi, Kitaramanka na Masurura vinavyohudumia wananachi wa maeneo hayo.
Leave a comment