MWILI wa aliyekuwa Mbunge Viti Maalumu (CCM), Mkoa wa Rukwa nchini Tanzania, Irene Ndyamkama, utazikwa mkoani Rukwa, Ijumaa ya tarehe 29 Aprili 2022. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatatu, tarehe 25 Aprili 2022, jijini Dodoma na Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson bungeni kabla ya kuahirisha shughuli za Bunge kwa mujibu wa kanuni hadi Jumatano, tarehe 27 Aprili mwaka huu, kwa ajili ya maombolezo ya msiba huo.
Spika Tulia amesema, mwili wa Ndyamkama utaagwa na wabunge keshokutwa- Jumatano bungeni kisha utazikwa mkoani Katavi.
“Kufuatia msiba huu, taarifa za awali ni kwamba, mwili wa marehemu utaletwa bungeni Jumatano, tarehe 27 Aprili 2022 kwa ajili ya kuagwa, mazishi yanatarajiwa kufanyika Ijumaa, tarehe 29 Aprili 2022 mkoani Katavi. Taarifa kuhusu msiba huu na jinsi tutakavyomuaga zitatolewa,” amesema Spika Tulia.
Spika Tulia amesema, marehemu Ndyamkama alifariki dunia jana Jumapili akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Tumbi, iliyoko wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani, baada ya kuugua ghafla akiwa safarini kuelekea Dar es Salaam na kulazimika kupelekwa hospitalini hapo.
Leave a comment