FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, amelazimika kutoa ufafanuzi wa kile kilichoonekana woga, baada ya kuomba muafaka kwa Rais John Magufuli. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Amesema, kilichompeleka Mwanza – kwenye sherehe za maazimisho ya Miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika – kwamba hawatavumilia hujuma zilizofanyika kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, zirudie katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
“Viongozi wa Chadema walikwenda jijini Mwanza, kwa ajili ya kutuma salamu kwa Serikali ya Rais John Magufuli, kwamba hawatavumilia tena hujuma zilizofanyika kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, zirudie katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani,” amesema.
Kwenye maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru wa Tanganyika tarehe 9 Desemba 2019 jijini Mwanza, Mbowe alisema “nimekuja kushiriki, kama uthibitisho wa ulazima kuwepo maridhiano, upendo na mshikamano kwa taifa letu. Tuvumiliane, tukosoane na turuhusu demokrasia; rais una nafasi ya kipekee kujenga maridhiano katika taifa.”
Kauli hiyo, ilishutumia vikali na baadhi ya wanasiasa wa upinzani, wafuasi wa upinzani na wawanaharakati kwamba, Mbowe ameingia woga na sasa amesalimu amri.
Hata hivyo, leo tarehe 12 Desemba 2019, akihutubia kwenye mkutano wa uchaguzi wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA), unaofanyika katika ukumbi wa Mliman City, jijini Dar es Salaam, Mbowe amesema Kamati Kuu ya chama hicho haikuwa na uoga, ilipokubali viongozi wake kwenda jijini Mwanza, kushiriki sherehe za uhuru.
“Kama Rais Magufuli na vyombo vyake vya ulinzi na usalama, wanafikiri watatufanyia walichofanya kwenye serikali za mitaa, mpatanishi atakuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Wako wengine wanaamini tungeyafanya hayo leo, lakini hamuwezi kufanya hivyo kama hamjajiandaa.
“Tutakaposema siku moja sasa twendeni, tusilaumiane. Nimewapa rai Mwanza juzi, nilishauriana na kamati Kuu (Chadema), hatukuwa wajinga na wala sio uoga.”
Mbowe amesema, Chadema inathamini tunu ya amani iliyopo, na kuikumbusha serikali kwamba, amani ni tawi linalotokana na msingi wa haki.
“Ila niseme, kila mmoja ana hubiri amani, sisi Chadema tunawaambia hatuna tatizo na kuhuibiri amani, lakini amani ni tawi ambalo linatokana na msingi wa haki. Kwa hiyo ambacho tunawataka watawala, tukianza kukiwasha, kukinukisha, tusilaumiane.
“Na kama wanafikiri watakuwa wanapambana na watu wanne walioko Dar es Salaam, watapambana nchi nzima kila kijiji, kitongoji na kaya. Kila jambo jema linahitaji maandalizi,” amesema Mbowe.
Pia amesema, hatamani tena siasa za mikutano ya hadhara, na kwamba anatamani siasa za nyumba kwa nyumba, kwa maelezo kwamba, njia hiyo inafaida na imekiimarisha chama chake.
“Leo mimi mwenyekiti wenu sitamani siasa za mikutano ya hadhara, natamani siasa za namba, wakati wa kugombea Uhuru, baba zetu hawakufanya mikutano ya hadhara. Ilipigwa marufuku na wakoloni, sheria ya leo ya uchochezi ni sheria ya kikoloni, leo watalawa wanatumia sheria hizo kupinga sisi kuwa na Uhuru wetu,” amesema Mbowe.
Leave a comment