FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa na wenzake, wamekutwa na kesi ya kujibu katika kesi ya jinai namba 112/2018, inayowakabili kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Leo tarehe 12 Septemba 2019, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema washtakiwa hao, kila mmoja ana kesi ya kujibu katika makosa 13 waliyoshtakiwa mahakani hapo.
Hakimu Simba ametoa uamuzi huo baada ya upande wa Jamhuri kupitia wakili Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi kuieleza mahakama hiyo kwamba imefunga ushahidi wake.
Baada ya Wakili Nchimbi kueleza hayo, Hakimu Simba amesema mahakama hiyo imepitia vielelezo saba na ushahidi wa mashahidi wanane wa Jamhuri uliowasilishwa mahakamani hapo, na kujitosheleza kwamba washtakiwa wana kesi ya kujibu.
Wadaiwa kwenye kesi hiyo ni Mbowe mwenyewe, Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu-Taifa; John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu – Bara na Salumu Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu -Z’Bar.
Wengine ni Ester Matiko Mbunge wa Tarime Mjini; Halima Mdee, Mbunge wa Kawe; Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini; John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini na Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.
Mbowe na wenzake wanatuhumiwa kufanya uchochezi wakati wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo katika jimbo la Kinondoni, kwenye viwanja vya Buibui na kisha kufanya maandamano.
Chadema walifanya maandamana hayo kupinga mawakala wao kutoapishwa kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo hilo. Tukio la maandamano hayo lilifanyika siku moja kabla ya siku ya uchaguzi huo tarehe 16 Februari 2018.
Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi tareje 17, 18 na 19 ambapo upande wa utetezi itaanza kuwasilisha utetezi wao.
Leave a comment