April 12, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe, wenzake hakijaeleweka

Spread the love

IKIWA ni siku ya kwanza ya kujitetea kwa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika kesi ya uchochezi namba 112/2018 kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kesi hiyo imeahirishwa. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Viongozi hao ni Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu wa chama; Salum Mwalim, Naibu Katibu Mkuu Chadema-Zanzibar; John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Chadema-Bara.

Wengini ni Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini; John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini; Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini; Halima Mdee, Mbunge wa Kawe na Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

Mahakama hiyo imeahirisha kesi hiyo kutokana na mtuhumiwa wa pili na wa nane kupatwa na msiba huku mawakili wengine wakipata dharura.

Mtuhumiwa wa pili ni Msigwa aliyedai mahakamani hapo kuwa, amefiwa na bibi yake huku mtuhumiwa wa nane, Heche akifiwa na mtoto wa ndugu yake.

Leo tarehe 17 Septemba 2019, Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Wakili Guston Garubindi aliyewawakilisha watuhumiwa hao, aliomba kuahirishwa kesi hiyo kwasababu:- mawakili wa utetezi wamepata wito katika Mahakama Kuuu mbalimbali kwenye mashauri mengine, sambamba na watuhumiwa kufikwa na msiba.

Kwenye shauri hilo, upande wa serikali umeongwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi, Dk, Zainab Mango na wakili  wa serikali Mwanamizi Wankyo Simon na wakili wa serikali Salum Msemo.

Garubindi amedai mahakamani hapo kuwa, wakili anayeongoza jopo hilo, Profesa Abdallah Safari yupo mbele ya Jaji Cyprian Mkeha katika Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga.

Pia, Peter Kibatala ameitwa kwa wito wa dharura Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Hekima Mwasipu yupo kwenye shauri katika Mahakama Kuu Kanda ya Tanga.

Baada ya kutoa ombi hilo, Wakili Nchimbi alipinga ombi hilo kwa  vile wito wa Kibatala ulimlenga wakili mwengine na kwamba kwake (Kibatala) umepitia tu.

“Hakuna wito  wa mahakama unaonesha Profesa Safari ameitwa Shinyanga kwa ajili ya kesi, kama amekwenda Shinyanga kumtembelea Jaji Mkeha tu!” amehoji.

Baadaye Hakimu Simba ameahirisha shauri hilo na kusema, litasikilizwa mfululizo tarehe 24 hadi 27 mwezi huu pia tarehe 1 mpaka 3 Oktoba mwaka huu.

error: Content is protected !!