August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe: Ukuta ni Oktoba

Spread the love

HAKUNA kurudi nyuma. Hii ndio kauli ya Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, anaandika Charles William.

Amesema, uamuzi wa chama hicho ni kusogeza mbele maandamano hayo ili kupisha mazungumzo baina ya Rais John Magufuli na taasisi mbalimbali nchini zilizoomba maandamano na mikutano hiyo kusogezwa mbele.

Amesema, Chadema kimeridhia maombi ya kusitisha maandamano na mikutano hiyo nchi nzima yaliyotolewa na viongozi wa dini mbalimbali, viongozi wa taasisi za kirai pamoja na Mama Maria Nyerere, mjane wa Mwalimu Julisu Nyerere.

Tarehe 27 Julai, mwaka huu Chadema kupitia Mbowe kilitangaza kuwa, Septemba 1 mwaka huu, kitazindua operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), ikiwa ni maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichoketi wa siku mbili.

Akizungumza na wanahabari leo, makao makuu ya chama hicho, Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mbowe amesema, Chadema inalazimika kuahirisha maandamano na mikutano ya kesho kutokana na kuheshimu wito wa viongozi wa dini zote waliowaomba.

“Viongozi wa dini zote hapa nchini kuanzia, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Mkuu wa Kanisa la Kianglikana Tanzania, Rais wa Baraza la Maaskofu (TEC), Katibu Mkuu wa Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), Mkuu wa Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT).

Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste (CPCT), Mufti Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) na Mufti Mkuu wa Zanzibar, wametusihi tuahirishe ili wao wazungumze na Rais John Magufuli kutafutia suluhu suala hili,” amesema Mbowe.

Mbowe amezitaja taasisi na watu wengine wenye heshima kubwa ndani na nje ya nchi waliokiomba chama hicho kuahirisha maandamano na mikutano hiyo kuwa ni Mzee Joseph Butiku ambaye ni Mwenyekiti wa Tasisi ya Mwalimu Nyerere, Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA),
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) pamoja na mjane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mama Maria Nyerere ambaye alizungumza na Edward Lowassa kwa niaba ya chama hicho.

“Kwa heshima ya viongozi wetu wa dini na taasisi hizi, tunawatangazia wanachama wetu kote nchini kuwa tunaahirisha maandamano hayo kwa muda wa mwezi mmoja ili kuwapa nafasi viongozi hawa waonane na Rais Magufuli na kama asipowaelewa hata hao, sisi tusilaumiwe,” amesisitiza Mbowe.

Aidha Mbowe amesema, Chadema haitishwi wala kutikiswa na maandalizi ya Jeshi la Polisi kote nchini, kwani wanaamini hakuna risasi na mabomu yaliyowahi kuishinda nguvu ya umma na kwamba maandamano hayo yataanza Oktoba ikiwa rais atawapuuza viongozi wa dini.

“Polisi na CCM wajue kuwa, hatuahirishi maandamano na mikutano yetu kwa sababu ya mazoezi, risasi au mabomu ya polisi. Hatiuahirishi kwasababu ya usafi wao wanaofanya kesho na wala hatuahirishi kwasababu ya ndege za kijeshi zinazoruka, ila tumeamua kuwaheshimu viongozi wetu dini,” amesema.

Tangu kutangazwa kwa operesheni Ukuta, serikali na kupitia Rais Magufuli; Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani; George Masaju, Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamekuwa wakitangaza kulaani na kupinga kufanyika kwa maandamano na mikutano hiyo.

Wengine kutoka serikalini waliojitokeza kupinga ni Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa, Nsato Marijani; Kamishina wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi pamoja na Wakuu wa Mikoa na Wilaya mbalimbali kote nchini.

………………………………………………………………………..

Soma gazeti la MwanaHALISI kila Jumatatu kwenye simu yako kupitia, (bonyeza)> Mpaper kwa wateja wa Vodacom pia (bonyeza)> Simgazeti kwa wateja wa Vodacom, Tigo na Airtel. Pia unaweza kupakua (download) app ya Mpaper au Simgazeti kutoka kwenye playstore.

error: Content is protected !!