FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema amesema, wanakwenda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 kuitafuta dola ili kuwaletea maisha bora na yenye furaha wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Mbowe ametoa kauli hiyo juzi Jumapili tarehe 28 Juni 2020 alipokuwa anazungumza na uongozi wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) na Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chaso) Mkoa wa Dar es Salaam.
Bavicha na Chaso walikwenda kumtembelea Mbowe nyumbani kwake Dar es Salaam anakoendelea kuuguza majeraha ya mguu wake unaodaiwa kushambuliwa na watu wasiojulikana.
Mbowe alifikwa na kadhia hiyo usiku wa kumkia tarehe 9 Juni 2020 akiwa anaingia nyumbani kwake Area D jijini Dodoma.
Akizungumza na vijana hao, Mbowe alisema Chadema haiendi katika uchaguzi huo, “kuomba kuwa chama kikuu cha upinzani, tayari sisi ni chama kikuu cha upinzani. Tunakwenda katika uchaguzi kuitafuta dola.”
“Hivyo vyama vingine, vinakwenda kuwatafuta wabunge na madiwani. Chama pekee nchini kinachoweza kusema kinakwenda kutafuta serikali ya Jamhuri ya muungano ni,” aliwauliza vijana hao na kujibiwa ‘Chadema.’
Mbowe alisema, wengine watapata wabunge watatu au madiwani wanne.

“Hatuitafuti dola kwa sababu ya tamaa ya madarakani, tunaitafuta dola kwa sababu ya hasira ya ndoto zetu ya kuibadilisha nchi hii kuwa nchi bora ya maisha, nchi ya furaha na nchi yenye haki,” alisema Mbowe huku akishangiliwa.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Tanzania alisema, wakishinda dola, watahakikisha usawa unakuwepo kwa kila mmoja bila kujali dini au kipato chake.
“Hatuendi kuitafuta dola ili kujenga madaraja na kununua ndege, tunakwenda kuitafuta dola tuleta furaha na maisha bora kwa watu wetu,” alisema
“Watu wetu wakishakuwa na maisha bora, wakishakuwa na furaha, haki ikawepo ndani ya taifa, amani ikawepo ndani ya taifa, ndege zitamnunuliwa, majengo yatajengwa na treni zitajengwa,” alisema.
Alisema lengo lao la msingi siyo kujenga barabara na kusahau haki za watu, furaha za watu na ustawi wa watu.
Mbowe aligusia suala la nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma akisema, miaka mitano imepita pasina nyongeza hiyo kwa, “mtumishi wa umma, wakati gharama za maisha zinapanda kutokana na mabadiliko ya mfumko wa bei unajiuliza serikali tuliyonayo si serikali ya watu?
Leave a comment