December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe na wenzake kortini kesho, Jaji anayesikiliza kesi hiyo kitendawili

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi nchini Tanzania, kesho Jumatano, tarehe 20 Oktoba 2021, inatarajia kutoa uamuzi wa kesi ndogo ndani ya kesi kubwa inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mahakama hiyo iliyopo Mawasiliano jijini Dar es Salaam, mbele ya Jaji Mustapha Siyani, tarehe 19 Septemba 2021, ilipanga kutoa uamuzi huo leo Jumanne, lakini imeahirishwa kutokana na Siku Kuu ya Maulid.

Bado haijafahamika kama Siyani ataendelea kusikiliza kesi hiyo au la baada ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kumteua na kumwapisha kuwa Jaji Kiongozi.

Jaji Kiongozi Siyani, amechukua nafasi ya Eliezer Feleshi ambaye aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Adelardus Kilangi ambaye aliteuliwa kuwa Balozi.

Mbali na Mbowe ambaye ni mshtakiwa wa nne, washtakiwa wengine katika kesi ya msingi ya uhujumu uchumi, yenye mashtaka ya kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi, ni Halfan Hassan Bwire (wa kwanza), Adam Kasekwa (wa pili) na Mohammed Abdillah Ling’wenya (wa tatu).

Kesi hiyo ndogo ndani ya kesi ya msingi, imetokana na mapingamizi ya upande wa utetezi, dhidi ya maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili, Kasekwa, yaliyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa jamhuri kama sehemu ya ushahidi wake.

Wakitaka yasitumike kwa madai yalichukuliwa kinyume cha sheria, ikiwemo mtuhumiwa kuchukuliwa maelezo hayo nje ya muda, bila ya ridhaa yake.

Na kwamba mahakama imepanga kutoa uamuzi dhidi ya kesi ndogo, baada ya pande zote mbili kuwasilisha ushahidi wake katika kesi hiyo ambapo jamhuri na utetezi walikuwa na mashahidi watatu kila mmoja.

Mashahidi wa utetezi walikuwa washtakiwa wawili kati ya wanne, Kasekwa na Ling’wenya, ambao walikamatwa pamoja tarehe 5 Agosti 2020, mkoani Kilimanjaro. Pamoja na Lilian Kibona, ambaye ni mke wa Kasekwa.

Katika utetezi wao, washtakiwa hao walidai walikamatwa, kuwekwa kizuizini na kuhojiwa na Jeshi la Polisi kinyume cha sheria ikiwemo kuchukuliwa maelezo nje ya muda was aa nne za kisheria pamoja na kuteswa.

Huku mshtakiwa wa pili, Kasekwa, akidai maelezo hayo ya onyo yanayobishaniwa mahakamani hapo, hakuyatoa yeye bali alipewa nyaraka zake na kulazimishwa azisaini pasina kujua kilichomo ndani yake.
Kwa upande wa jamhuri, mashahidi walikuwa ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kinondoni, Dar es Salaam, ACP Ramadhan Kingani, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Arusha, wakati washtakiwa hao wanakamatwa.

Kwa sasa, Kingai ni Kamanda wa Polisi Kinondoni, Dar es Salaam.

Wengine ni, aliyekuwa Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Arusha, Mahita Omari Mahita na Detective Ricado Msemwa, aliyewapokea watuhumiwa hao walipofikishwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam, wakitokea Kituo cha Polisi cha Kati Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Mashahidi hao wa jamhuri walitoa ushahidi wao mahakamani hapo wakidai kuwa, maelezo hayo ya onyo ni halali, kwa kuwa taratibu za kisheria zilifuatwa wakati mshtakiwa huyo anahojiwa.

error: Content is protected !!