Friday , 29 March 2024
Habari za SiasaTangulizi

Mbowe: Msiogope

Spread the love

FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amewataka Watanzania waliosimama na upinzani katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2020, wasiogope. Anaripoti Mwamdishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Akizungumza katika salamu zake za mwaka mpya 2021, jana Jumatatu tarehe 4 Januari 2021, Mbowe amesema, ingawa wengi wameumizwa na wengine wanaendelea kuumia, lakini wasikate tamaa.

“Nawashukuru Watanzania wote mlioongozwa na watoa huduma za kiroho, mliokuwa na ujasiri wa kusimama upande wa haki wakati wote kabla na baada ya uchaguzi.”

“Hakika wengi mlikesha na kuomba na hata kutuunga mkono kwa hali na mali kipindi chote cha uchaguzi, wengi mmeumizwa, na wengine bado mnaumizwa na wengine mtaendelea kuumizwa. Nawasihi wote kwa pamoja, msiogope,” amesema.

Kiongozi huyo wa upinzani amesema, Taifa limeshuhudia uchafuzi katika uchaguzi uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, kama ilivyofanyika kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019.

Na kwamba, mwaka 2020 ulikuwa na majaribu mengi kwake, kwa familia yake na familia ya Chadema lakini Mungu amewezesha mwaka huo kupita salama.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu kupita kwenye mwaka uliokuwa wa majaribu mengi kwangu binafsi, kwa familia yangu na bila kusahau familia nzima ya Chadema. Ni kwa mamlaka na uweza wake (Mungu) kwamba, pamoja na nguvu kubwa na hila za watesi wetu, bado wanaendelea kusikia sauti zetu.”

“Miongoni mwetu wapo walioathirika zaidi, wapo waliopoteza maisha…, wapo walioshitakiwa kwa uonevu usio kifani na wengine bado wanataabika magerezani. Wako waliojeruhiwa kimwili na hata kisaikolojia, watabaki kama kumbukumbu ya kishujaa waliopigania kesho yetu bora,” amesema Mbowe.

Akizungumzia ushindani wa tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema, chama hicho tayari kinajua kwamba hakiwezi kupambana tena na hakikubaliki katika maeneo mengi ya nchi.

“CCM hawana uwezo wa kushinda uchaguzi ulio huru na haki katika maeneo mengi ya nchi yetu,” amesema na kuongeza “Lissu (Tundu Lissu aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema) alikuwa mgombea bora aliyesheheni hoja zote.”

Kwenye salamu hizo, Mbowe amesema, Watanzania kwa muda mrefu wana ndoto ya Uhuru, Haki na Maendeleo ya kweli kuliko porojo za kukua kwa uchumi.

“Chadema ni tumaini la wengi la kesho bora na sio jukwaa la propaganda kama ilivyozoeleka,” amesema.

Mbowe ameeleza mashaka yake kuhusu data zilizomo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kwamba halifai kutumika katika chaguzi zijazo.

Kiongozi huyo amesema, Daftari la Kudumu la Wapiga Kura limevurugwa, hivyo linahitaji marekebisho makubwa ili libebe idadi sawa na wapiga kura waliopo.

“Daftari la Kudumu la Wapiga Kura limevurugwa sana kiasi cha kukosa uhalali wa kutumika katika chaguzi zijazo na linastahili kuandikishwa upya kwa usimamizi uliokuwa huru,” amesema.

Amesema, chama hicho kilishiriki uchaguzi mkuu kikitambua mazingira magumu yaliyopo na kuwa, kilifanya hivyo ili kuuthibitishia umma kwamba, chama hicho bado kipo imara.

“Chadema kilishiriki uchaguzi huo tukijua ugumu wa upatikanaji wa haki kutokana na mazingira hatarishi yaliyojengwa katika miaka mitano iliyopita.

“Tulitaka kuwadhihirishia wanachama wa Chadema kwamba, pamoja na kushughulikiwa sana, bado kiko imara na kiko tayari kuongoza ukombozi wa pili wa Taifa letu,” amesema.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!