August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe, Lowassa, Lissu ‘wavamia’ polisi

Spread the love

FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chma cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiambatana na viongozi wengine wa chama hicho leo mchana ameitikiwa wito wa Jeshi la Polisi, anaandika Faki Sosi.

Mbowe juzi aliandika kwenye ukurasa wake wa instagram kwamba, ameitwa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa mahojiano maalumu.

“Ndio, ameitikia wito kama alivyotakiwa na Jeshi la Polisi na kwa sasa wapo ndani wanaendelea,” ameeleza Tumaini Makene, Ofisa Habari wa Chadema.

Amesema, Mbowe ameongozana na viongozi mbalimbali wa chama hicho akiwemo Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara.

Wengine ni Tundu Lissu, Mwanasheria wa Chadema, Hashim Issa Juma, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema.

Ofisa huyo wa habari amesema, kwa sasa sio rahisi kujua nini kinazungumzwa kwa kuwa “kwenye wito wao hawajaeleza nini hasa wanahitaji. Inatulazimu kusubiri mpaka watakapotoka.”

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku chache tangu Rais John Magufuli na Chadema kupishana kauli kuhusu zuio la mikutano ya hadhara ya kisasa nchini.

Rais Magufuli alitoa agizo la kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa nchi nzima jambo ambalo limekuwa likipingwa na vyama vya upinzani, baadhi ya wabunge wa CCM pamoja na wananchi.

Hatua ya kuzuia mikutano hiyo inaelezwa kulenga kufifisha ustawi wa demokrasia nchini jambo ambalo limesababisha kupingwa na kada mbalimbali nchini.

Upinzani umekuwa ukishutumu Serikali ya Rais Magufuli kwamba, ina lengo hasi kuhusu la kuua vyama vya upinzani nchini.

Mara kadhaa imekuwa ikikosoa kauli zake dhidi ya upinzani na kwamba, mwelekeo wake unalenga zaidi kuua demokrasia kinyume na mtangulizi wake Dk. Jakaya Kikwete.

Hatua kadhaa alizochukua Rais Magufuli zimekuwa zikiibua malumbano kwa wapinzaji na wananchi ikiwa ni pamoja na kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge, namna anavyotumbua watumishi wa serikali.

Pia namna anavyoelekeza fedha za sherehe za kitaifa katika matumizi mbalimbali, kuzuia kuingiza sukari nchini pamoja na kuzuia mikutano ya kisiasa.

 

error: Content is protected !!