December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe kung’oka? Mchakato waanza

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

MCHAKATO wa kupata viongozi mbalimbali wapya ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umetangazwa kuanza rasmi. Anaripoti Hamis Mguta … (endelea).

Akizungumzia kuanza kwa mchakato huo, Dk. Vincent Mashinji, katibu mkuu wa chama hicho leo tarehe 18 Novemba 2019, amewataka wagombea kuanza kuchukua fomu ili kukamilisha mchakato huo.

Nafasi ya uenyekiti wa chama hicho – Taifa inayokaliwa na Freeman Mbowe, ni miongoni mwa nafasi zinazogombewa kwenye uchaguzi huo wa ndani.

Tayari tayari Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda alitangaza dhamira ya kuitaka nafsi ya uenyekiti wa chama hicho Taifa akisema, wakati umefika kwa Mbowe kuwaachia wengine nafasi hiyo, baada ya kuishikilia kwa muda mrefu.

“Tunamshukuru kwa mchango wake alioutoa katika chama chetu, lakini nadhani umefika wakati wa kuwaachia kiti wengine,” alisema Mwambe.

Mbowe alianza kuongoza chama hicho mwaka 2004, kutoka kwa aliyekuwa mwenyekiti wake Bob Makani. Makani alifariki dunia tarehe 10 Juni 2012.

Ndani ya Chadema, kampeni za kutaka Mbowe aendelee kuwa mwenyekiti wa chama hicho, zimekuwa zikifanywa mkoa kwa mkoa zaidi ya mwezi mmoja uliopita.

Dk. Mashinji amesema, mbali na nafasi ya uenyekiti –Taifa, nafasi zingine zinazogombewa ni makamu wenyeviti wawili – Taifa, (mmoja Bara na mwingine visiwani), wajumbe wanae wa Kamati Kuu (sita kutoka Bara na mbili visiwani).

“Kuna nafasi zitakazogombewa kwenye mabaraza matatu ya chama hicho ambayo ni Wazee, Wanawake na Vijana. Hapo kila mwenyekiti atakuwa na makamu wawili –Bara na Visiwani, Katibu wa Baraza Taifa, Naibu Katibu Tanzania Bara na mwengine Zanzibar,” amesema.

Dk. Mashinji amesema, kutoka katika mabaraza hayo, kuna nafasi ya mweka hazina, wajumbe watano wawakilishi wa Baraza Kuu la Chama na wajumbe 20 wawakilishi wa mkutano mkuu wa chama Taifa.

“Mwisho wa kuchukua fomu ni tarehe 30 Novemba 2019, wanachama wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa juu wa chama, wanze kuchukua fomu kuanzia leo.

“Kamati Kuu itakutana ili kuchuja na kupitia majina ya walioomba nafasi mbalimbali kwa ajili ya uteuzi, tarehe 10 Desemba tutakuwa na kikao cha kamati tendaji ya Baraza la Wazee, na kikao cha kamati tendaji cha Baraza la Vijana,” amesema.

Amesema, tarehe 11 kutakuwa na kamati tendaji ya BAWACHA na baada ya hapo, kutakuwa na kikao cha Kamati Kuu ili kufanya uteuzi wa viongozi ngazi ya taifa.

“Tarehe 17 kutakuwa na mkutano mkubwa wa Baraza Kuu la chama, kuteua wagombea nafasi ya uenyekiti na makamu wake ambapo tarehe 18 uchaguzi utafanyika,” amesema.

Amesisitiza, Chadema hakipo kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu, hivyo hawategemei kuhusishwa wala kuulizwa yanayoendelea katika uchaguzi huo.

error: Content is protected !!