June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe kukosa mazishi ya baba yake mdogo

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, atashindwa kuhudhuria mazishi ya baba yake mdogo, Manase Mbowe, aliyefariki dunia tarehe 23 Julai 2021, mkoani Kilimanjaro. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mbowe atashindwa kuhudhuria mazishi hayo, kutokana na kuwa mahabusu katika Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam, anakoshikiliwa kwa tuhuma za ugaidi.

Akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu, leo tarehe 27 Julai 2021, Mtoto wa Mbowe, James Mbowe, amesema mazishi ya Manase yanatarajiwa kufanyika Machame mkoani Kilimanjaro, kesho tarehe 28 Julai 2021.

“Kitendo cha kupelekwa mahakamani na kusomewa mashtaka ya ugaidi ambayo huwa hayana dhamana na kumbuka hilo jambo kwa sasa lipo mahakamani na kuomba ruhusa,” amesema James.

Mbowe alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, jana tarehe 26 Julai 2021 na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi na ugaidi.

Kwa mujibu wa mashtaka hayo, Mbowe anadaiwa kula njama na kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi.

Mwanasiasa huyo alisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba, na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ester Martin, akisaidiwa na Tulimanywa Majigo.

Inadaiwa kuwa, Mbowe alitenda makosa hayo kati ya Mei na Agosti 2020, kwenye Hoteli ya Aishi, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kesi ya Mbowe, inatarajiwa kusikilizwa tena tarehe 5 Agosti 2021, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha nyaraka muhimu katika Mahakama Kuu, kwa ajili kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Mbowe alifikishwa mahakamani siku tano, tangu alipokamatwa akiwa katika Hoteli ya Kingdom jijini Mwanza, usiku wa kuamkia tarehe 21 Julai mwaka huu, akijiandaa kushiriki kongamano la kudai katiba mpya.

error: Content is protected !!