Tuesday , 18 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mbowe kufikishwa kwa msajili
Habari za Siasa

Mbowe kufikishwa kwa msajili

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema
Spread the love

VYAMA nane vya siasa nchini Tanzania, vimelaani kauli iliyotolewa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema kuvituhumu kwamba vinatumika kurudisha nyuma mapambano ya kupigania haki na demokrasia nchini humo. Anaripoti Mwandishi, Dar es Salaam …(endelea).

Vyama hivyo vimemwomba msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mtungi kuitisha kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa ili Mbowe aliyewahi kuwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni athibitishe kauli hiyo.

Jumapili ya tarehe 4 Oktoba 2020, Mbowe akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam alisema, baadhi ya vyama vinatumika vibaya.

Mbowe alisema hayo wakati akitoa maazimio ya kikao cha dharura cha kamati kuu kilichokuwa kikijadili uamuzi wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumfungia kwa siku saba, Tundu Lissu, mgombea urais kupitia chama hicho kutokufanya kampeni.

Lissu alifungiwa kuanzia 3 hadi 9 Oktoba 2020 baada ya vyama vya NRA na CCM kumlalamikia kutoa maneno ya uchochezi yasiyothibitika.

Kamati hiyo ya maadili inahusisha vyama 15 vilivyosimamisha wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano 28 Oktoba 2020.

Mbowe alisema, hakuna ubishi kwamba katika uchaguzi huu, ni wagombea wawili pekee wenye nguvu ambao ni Tundu Lissu na Rais John Pombe Magufuli wa CCM, hivyo vyama vingine vinaposhiriki mpango wa kumfungia Lissu siku saba si sahihi.

Leo Jumatano, tarehe 7 Oktoba 2020, vyama hivyo nane ambavyo ni; ADC, NRA, AAFP, DP, UMD, UPDP, SAU na Demokrasia Makini vimezungumza na waandishi wa habari mkutano huo umehudhuriwa na wagombea wenza wa vyama hivyo.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Katibu Mkuu wa DP, Abdul Mluya amesema, sheria ya vyama vya siasa, inawatambua kwa usawa bila kujali nani mkubwa au mdogo na ndiyo maana kila mmoja anashirikishwa kwa kila jambo.

“Kauli iliyotolewa na Mbowe akivituhumu vyama vilivyopo kwenye kamati ya maadili ya NEC ambayo ilitoa hukumu dhidi ya Tundu LIssu kuwa vinatumika, ana waaminisha Watanzania vyama hivi havifanyi siasa.”

“Hawajui CUF, Chadema, ACT na CCM wanapata ruzuku sisi hatuna ruzuku na hili lazima alijue. Sisi tunaendesha kampeni kwa kutoa fedha zetu mfukoni au kuchangishana changishana. Ni haki yetu kisheria na Mbowe anapaswa kufahamu vyama hivi vimesajiliwa kisheria isipokuwa sehemu moja tu sisi hatupati ruzuku,” amesema Mluya.

“Anaposema kiongozi mkubwa kama yeye aliyewahi kuwa kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani si matusi kwa vyama bali kwa Watanzania. Hawezi kusema sisi tunatumika, hii si sawa kabisa,” amesema.

Mluya amesema “hili jambo tutalipeleka ofisi ya msajili ili aite baraza la vyama ili Mbowe aje athibitishe anachokisema.”

Amesema, kila chama kinashindanisha sera kwa wananchi ili kuwezesha kuwashawishi wawachague na si kutumia maneno ya vitisho, kejeli au uchochezi.

Naye Katibu Mkuu wa AAFP, Rashid Rai amesema, uchaguzi ni jambo la kisheria kwamba uongozi utakuwa na kipindi cha muda fulani Fulani ambapo Tanzania huwa ni miaka mitano.

“Unapofika wakati wa uchaguzi, linakuwa si jambo la mtu bali ni la Watanzania wote na mtu yoyote akifanya jambo linalokwenda kinyume na hilo inakuwa ni makosa.”

“NEC imeweka maadili ambayo vyama vyote 19 vinavyoshirikii uchaguzi vimesaini kikiwemo Chadema, sasa mgombea wake anapokwenda visivyo na kuadhibiwa halafu Mbowe anatutuhumu sisi kwamba tunatumika, tunakuwa hatumwelewi,” amesema Rai

Rai amesema, Lissu kama ameshindwa kufanya siasa aache kwani kuongoza nchi si jambo lelemama na wafanye siasa bila kuvihusisha vyama vingine

“Kama tumewekeana utaratibu huu, halafu tunakwenda kinyume na hapo ni kasoro, ninachokiona mimi ni Chadema, Tundu Lissu na wafuasi wao wanakwenda kinyume na hicho, naona kama pumzi imekata, sasa wasitafute mchawi wapambane na hali yao” amesema

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mazingira magumu ya JPM yamechangia ‘Comedy Journalism’

Spread the loveMwenyekiti wa Kamati ya kufuatilia hali ya uchumi wa vyombo...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

RC Chalamila: Nimeacha ubabe

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chamalila amemthibishia...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia atoa ujumbe mzito Sikukuu Eid Al Adha

Spread the loveKATIKA kusherehekea Sikukuu ya Eid Al Adha, Rais wa Tanzania,...

BiasharaHabari za Siasa

Dk. Biteko aipongeza NMB kwa kuanzisha utoaji wa bima ya mifugo

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!